Friday 25 February 2011

13bn/ kuimarisha kilimo, mifugo Z’bar

13bn/ kuimarisha kilimo, mifugo Z’bar



Na Mwanajuma Abdi


ZAIDI ya dola za Marekani milioni tisa sawa na shilingi bilioni 13.391 zitatumika katika mradi wa kuimarisha na kuendeleza huduma za kilimo na mifugo ASSP/ASDP-L Zanzibar ili kusaidia kupambana na umasikini na kuwepo uhakika wa chakula.

Hayo yalifahamika jana, wakati Mratibu wa Mradi Zaki Khamis Juma alipokuwa akiwasilisha ripoti ya utekelezaji wa programu za ASSP/ASDP-L kwa mwaka 2010 katika mkutamo wa kutathmini utekelezaji wa miradi hiyo kwa wadau wa kilimo na mifugo, uliofanyika Maruhubi mjini hapa.

Alisema miradi hiyo imeanzishwa mwaka 2007, ambapo lengo lake ni kupunguza umasikini na kuwepo kwa uhakika wa chakula na kuongeza kipato kwa jamii zinazotegemea kilimo.

Mradi wa ASSP, utatumia dola za Marekani milioni 5.9777, ambao utarajiwa kukamilika mwezi Machi mwaka 2014, wakati mradi wa ASDP-L, utagharimu dola za Marekani milioni 3.76, na utakamilika 2015.

Alieleza miradi hiyo imekusudia kuwanyanyua wakulima wakiwemo wanawake na masikini wa vijijini kwa kuwawezesha kitaaluma ili kuzitumia teknolojia za kilimo zitazochangia kutosheleza chakula na kipato.

Aidha alitoa wito kwa watu binafsi wenye uwezo kuwekeza katika kilimo badala ya kuwekeza katika maduka na vituo vya mafuta, kwani kufanya hivyo kutasidia kukuza uchumi kupitia sekta hiyo.

Nae Katibu wa Baraza la Wakulima Mkoa wa Kusini Unguja, Mashavu Juma, alisema changamoto kubwa zinazowakabili ni wizi wa mazao na mifugo ambazo bado ni matatizo sugu katika wilaya hususan wanyama kama ng’ombe.

Alieleza changamoto nyengine ni uhaba wa maji na malisho kwa wafugaji na wakulima, wanyama waharibifu kama kima na vifo vya kuku.

Mapema akifungua mkutano huo wa siku moja Mkurugenzi wa Idara ya Utumishi na Uendeshaji wa Wizara ya Kilimo na Maliasili, Asha Ali Ameir, alisema Serikali katika kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara imeandaa mipango na mikakati mbali mbali yenye lengo la kuongeza uzalishaji, kuinua kipato cha wakulima, wafugaji na wavuvi.

Mipango hiyo inalengo la kufikia malengo ya millennia ya Umoja wa Mataifa, Dira ya Maendeleo ya 2020 na Mpango Mkuu wa Kupunguza Umasikini Zanzibar (MKUZA) ambayo dhamira kuu ni kumoundoa mkulima kutoka katika uzalishaji duni na kuelekea katika uzalishaji wenye tija.

Kuna vikundi 360 vinavyowakilisha kaya 6,675 katika wilaya tisa Unguja na Pemba, ambavyo vimepatiwa mafunzo katika skuli za wakulima.

No comments:

Post a Comment