Wednesday 23 February 2011

DENI LA MUNDU LAIKAANGA ZFA

Deni la Mundu laikaanga ZFA

 Latumiwa kumkacha mjumbe wake safari ya Z’bar Ocean
Na Salum Vuai, Maelezo

KATIKA hali isiyotarajiwa, timu ya Zanzibar Ocean View iliondoka jana kwenda DR Congo kurudiana na klabu ya AS Vita bila kuambatana na mjumbe wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA).

Mwandishi wetu alishuhudia kikosi cha wachezaji 16 na viongozi wanne wa timu hiyo kikiingia uwanjani kwa ajili ya kupanda ndege ya Shirika la Kenya Airways bila mjumbe wa chama hicho.

Kwa kawaida mjumbe wa ZFA anapaswa kufuatana na msafara wa klabu inayoiwakilisha nchi kwenye michuano ya klabu barani Afrika, ili iwapo kutatokezea tatizo lolote aweze kulishughulikia.

Baada ya jitihada za kumpata Msaidizi Katibu wa ZFA Masoud Attai kushindikana kwa kuwa simu zake mbili zilikuwa zimezimwa kwa muda mwingi, Mjumbe wa Sekretarieti ya chama hicho Mussa Soraga, alisema kuondoka bila mjumbe wa ZFA ni kosa kwa mujibu wa kanuni.

Hata hivyo, uchunguzi wa gazeti hili umebaini sababu iliyoifanya Zanzibar Ocean isichukue mjumbe wa chama hicho katika safari yake, ni kutolipwa deni la shilingi 5,000,000 inaloidai ZFA.

Imefahamika kuwa wakati klabu ya Mundu iliyokuwa ikishiriki michuano ya Kombe la CAF iliposhindwa kulipia hoteli iliyofikia timu ya Red Arrows ya Zambia mwaka juzi mjini Dar es Salaam, deni hilo lililipwa na hoteli ya Zanzibar Ocean View huku ZFA ikibeba dhamana ya kurejesha fedha hizo.

Barua iliyotumwa kwa chama hicho ambayo Katibu Mkuu wa Zanzibar Ocean View aliionesha Zanzibar Leo nakala yake, ilieleza kuwa, ili mjumbe wa ZFA aweze kusafiri, chama hicho kimeruhusiwa kitoe dola 1,000 katika deni inalodaiwa, kwa ajili ya kumnunulia tiketi mjumbe wake.

Kupitia barua hiyo, uongozi wa Zanzibar Ocean ulikiambia chama hicho kwamba kutokana na hali ya fedha kuwa mbaya, wadhamini wamemudu kusafirisha idadi ya watu 20 tu ambao ni wachezaji 16 na viongozi wanne bila kuwemo mjumbe wa ZFA.

Hata hivyo, kutokana na ukata unaokikabili, chama hicho kimekosa fedha na kuamua kulinyamazia suala hilo.

Kuhusu kadhia ya kuwepo deni hilo, Soraga alisema halifahamu na kuliahidi gazeti hili kulipatia taarifa baada ya kulifanyia utafiti.

No comments:

Post a Comment