Tuesday, 1 February 2011

DK. BILAL AHIMIZA WAFANYABIASHARA UTURUKI KUWEKEZA NCHINI.

Dk. Bilal ahimiza wafanyabiashara Uturuki kuwekeza nchini


Mwandishi Maalum, Dar es Salaam


MAKAMU wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal amehimiza wafanyabiashara wa Uturuki kuwekeza nchini Tanzania ili waweze kunufaika na soko la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Dk. Bilal alitoa kauli hiyo jana alipozungumza na Balozi wa Uturuki nchini, Dk. Sander Gurbuz ambaye alimtembelea ofisini kwake Ikulu, Jijini Dar es salaam.

Alisema amefurahi kusikia Uturuki imetambua kuna fursa za biashara nchini na kusema kwa vile Tanzania ina uhusiano mzuri na majirani zake wafanyabiashara wa nchi hiyo watapata fursa pia ya kutumia soko hilo kubwa na la aina yake.

“Nimefurahi kusikia serikali ya Uturuki imetambua kuna fursa za biashara nchini. Tanzania ni mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki yenye watu zaidi ya milioni 120 na Tanzania ni nchi pekee ambayo inaaminika kuwa na amani,” alisema Dk. Bilal na kuongeza

“Nje ya EAC, tuna uhusiano mzuri pia na nchi za SADC. Hivyo kwa kuwekeza na kufanya biashara Tanzania, wafanyabiashara kutoka Uturuki watanufaika na soko hilo kubwa la EAC na SADC.”

Katika mazungumzo hayo, Dk. Sander Gurbuz alimweleza Makamu wa Rais kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu toka Ubalozi wa Uturuki uanzishwe nchini, akiwa kama Balozi wa kwanza ameweza kufanikisha mambo mbalimbali yanayolenga kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na Uturuki.

Alisema katika kipindi hicho ameweza kufanikisha safari za viongozi wa kitaifa wa nchi hizo mbili, shirika la ndege la Uturuki limeanza safari zake nchini na mikataba mitano ya ushirikiano imetiwa saini iliyowawezesha wafanyabiashara wa Uturuki wameanza kuja Tanzania kuwekeza katika maeneo mbalimbali kama ya madini, utalii na kilimo.

Hivi sasa ujumbe wa watu wapatao 7 wamewekeza katika maeneo ya migodi iliyoko wilayani Mpanda mkoa mpya wa Katavi na wengine wako Zanzibar ambako wanashughulikia Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Zanzibar.

Aidha, alisema katika jitihada za kuimarisha ushirikiano wa nchi mbili hizi Spika wa Bunge la Uturuki anatarajia kuitembelea Tanzania hivi karibuni na hali kadhalika mwezi ujao Waziri wa Biashara wa Uturuki ataongoza ujumbe wa wafanyabiashara wapatao 100 kutembelea Tanzania kwa madhumuni ya kujadiliana namna ya kushirikiana kiuchumi.

No comments:

Post a Comment