Dole wamwagiwa jezi, mipira
Na Saada Mamboleo, MCC
MBUNGE na Mwakilishi wa Jimbo la Dole Syllvester Mabumba na Shawana Bukheti Hassan, wamezipa msukumo timu 22 za soka katika wadi ya Mwera, kwa kuzikabidhi jezi na mipira ili kuzipa motisha wa kufanya vyema katika mashindano mbalimbali.
Mipira 44 na seti 22 za jezi zenye thamani ya shilingi 3,438,000 zilitolewa katika hafla iliyofanyika skuli ya Regezamwendo juzi.
Makabidhiano hayo ni miongoni mwa utekelezaji wa ahadi zilizotolewa na Mbunge huyo wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka jana.
Akizungumza na wanamichezo wa timu hizo wakati wa kukabidhi vifaa hivyo, Mabumba aliwashauri vijana wa jimbo la Dole, kuendeleza utamaduni wa kushiriki michezo mbalimbali na kujiepusha na vitendo viovu.
Aliwapongeza vijana hao kwa kuamua kuanzisha timu za soka, na kuongeza kuwa hatua hiyo itasaidia kuimarisha afya zao na kujijengea maisha bora hapo baadae.
Mapema Mwakilishi wa jimbo hilo Shawana Bukhet Hassan, alisema ni lazima michezo isimamiwe kwa hali na mali ili kuijengea Zanzibar mustakbali mzuri kitaifa na kimataifa, na kuzitaka timu hizo kuvitumia vizuri vifaa hivyo ili hatimaye zifike ligi kuu ya Zanzibar.
Mwenyekiti wa michezo wadi ya Mwera Gharib Suleiman Omar, amewashukuru viongozi hao na kusema wamefurahishwa na msaada huo na watautumia kwa malengo yaliyokusudiwa.
Sunday, 27 February 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment