Tuesday, 1 February 2011

MZAHA DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA UTAANGAMIZA TAIFA ; MAALUM SEIF.

Mzaha dhidi ya dawa za kulevya utaangamiza Taifa: Maalim SeifNa Abdi Shamnah, Pemba

MAKAMU wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, amezitaka taasisi za Serikali, vyombo vya Ulinzi na Usalama, kushikamana katika harakati za kupiga vita uingizaji wa dawa za kulevya.

Amesema uingizaji na matumizi ya dawa za kulevya ni vita na suala la mapambano ya Taifa, na kuonya kuwa pale litakapofanyika mzaha, ni wazi kuwa linaweza kuangamiza nguvu kazi ya Taifa.

Maalim Seif, ameyasema hayo leo, Machomane Pemba, alipozungumza na wafanyakazi wa Idara zilizo chini ya Ofisi yake, ikiwa ni muendelezo wa ziara zake kutembelea Ofisi hizo na kupata taarifa za utendaji pamoja na changamoto mbali mbali zinazowakabili.

Alisema katika mapambano hayo mkazo zaidi unahitajika kuelekezwa katika kukinga, kwa kujenga ushirikiano na Wananchi ili kuwafichua waingizaji na wasambazaji wa dawa hizo.

Aidha alielekeza umuhimu wa wananchi kuelimishwa juu ya madhara ya dawa za kulevya, sambamba na kuwa tayari kushiriki katika Ulinzi shirikishi.

Maalim Seif aliagiza kitengo cha Utoaji na Elimu kaika Idara hiyo kufanya kazi ya ziada ya kuwafikia wananchi popote pale walipo, iwe mjini au vijijini.

Alisisitiza umuhimu wa kuwepo uaminifu huruma kwa waathirika na uzalendo katika utekelezaji wa kazi hiyo, kwa kigezo kuwa maadui wakubwa katika vita hivyo ni watu wenye uwezo mkubwa kifedha.

Alisema Serikali itafanya kila iwezalo kuhakikisha masuala ya nyenzo, taaluma pamoja na usafiri, yanapatiwa ufumbuzi kadri hali itakavyoruhusu.

Akizungumzia suala la watu wenye ulemavu, Maalim Seif alisema, Serikali inajali jamii hiyo kwa kuwa na haki sawa kama ilivyo jamii nyengine na kutaka kuwepo takwimu sahihi ili Taifa liweze kupanga mipango yake ya kuisaidia jamii hiyo pamoja na kuelewa mahitaji yao kwa kila kundi.

Alionya ulemavu kutotumika kama kigezo cha kuikosesha jamii hiyo haki, ikiwemo fursa za ajira na kuagiza majengo yote ya utoaji wa huduma lazima yawe na visaidizi.

Aidha alisema ni lazima kuwepo na mipango na mikakati madhubuti katika mapambano dhidi ya ukimwi na kutaka mkazo zaidi kuelekezwa katika kuzuia maambukizo mapya ya ugonjwa huo.

Alisema suala la elimu kwa jamii ni muhimu, ili kuhakikisha ujumbe umefika kwa walengwa na kutaka uwepo umuhimu katika kurudisha maadili mema ya wazanzibari.

Maalim Seif alisisitiza umuhimu wa kulinda mazingira na kusema mabadiliko makubwa ya hali ya hewa, kumetokana na uchafuzi wa mazingira kufuatia vitendo vinavyofanywa na binaadamu.

Alikemea wimbi la uingizaji wa bidhaa kutoka nje, hususan zile za Electronic na kumainisha kuwa ni kiwango kidogo tu ndio zenye kufaa kwa matumizi.

Alikipongeza kikosi cha KMKM katika kukabiliana na uharibifu huo wa kimazingira, kufuatia tukio la kukamata Tani 40 ya mifuko ya Plastik.

Aidha amerudia kauli yake na kukemea matumizi ya misumeno ya moto, na kusema Kisiwa cha Pemba kimo hatarini kupoteza mandhari yake iwapo hatua thabiti zitasita kuchukuliwa kwa haraka na kwa nguvu zote.

Mapema Mkuu wa Mkoa Kusini Pemba Juma Kassim Tindwa aliwatka watendaji wa Idara hizo kujenga mashirikiano na viongozi wa Serikali katika ngazi zote, wakielewa wana kazi kubwa katika kusimamia utendaji wa Idara zao. Nao baadhi ya wafanyakazi wa Idara hizo walimueleza Makamo wa Kwanza wa Rais juu ya changamoto zinazowakabili ikiwemo ufinyu wa Ofisi, vitendea kazi pamoja na mahitaji ya Taaluma kwa watendaji.

No comments:

Post a Comment