Friday 25 February 2011

Wanafunzi Kengeja wahaha kusaka walimu

Wanafunzi Kengeja wahaha kusaka walimu

Radhia Abdalla, Pemba

WANAFUNZI wa Chuo cha Ufundi Kengeja wamefika katika Afisi za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Pemba kutaka wapatiwe ufumbuzi wa tatizo la walimu linaloikabili chuo hicho, ambalo wanadai ndio chanzo cha wanafunzi kufanya vibaya katika mitihani ya kitaifa.

Wakizungumza na afisa wa huduma za wanafunzi wa Sekondari, Said Massoud Othman, wanafunzi hao walisema chuo hicho kinakabiliwa na upungufu mkubwa wa walimu hali inayoathiri kwa kiasi kikubwa wanafunzi.

Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake wa kidato cha nne, raisi wa skuli hiyo, Ali Kombo alisema tatizo hilo linawakatisha tamaa hasa wakati huu ambapo wanakabiliwa na mitihani ya kitaifa mwishoni mwa mwaka huu

“Tunalazimika kujisomea sisi wenyewe bila ya kuwa na walimu wa uhakika kwani mwalimu mmoja hulazimika kufundisha zaidi ya madarasa matatu kwa siku na masomo matatu kwa kila siku,” alisema.

Alisema hali hiyo inawafanya walimu kutokuwa na umakini wawapo madarasani kutokana na kukosa muda wa kujitayarisha vyema na kupumzika.

Alisema licha yaskuli hiyo kuwa ndio iliyokuwa ikiongoza kwa kupasisha wanafunzi, lakini kwa sasa inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa nipamoja na upungufu wa walimu.

Aliyataja matatizo mengine kuwa ni uhaba wa vitabu, vifaa vya masomo kwa vitendo, uhaba wa madarasa na ufinyu wa mabweni ya kulala wanafunzi.

“Kwa mfano mabweni yaliopo yana uwezo wa kuchukua wanafunzi 56 lakini kwa sasa yanatumiwa na zaidi ya wanafunzi 150,” alifafanua rais huyo.

Akijibu malalamiko ya wanafunzi hao, afisa huyo kutoka wizara ya elimu Pemba, alisema serikali itafanya jitihada ili kuhakikisha kuwa walimu wanapatikana kuondoa tatizo katika kipindi kifupi kijacho.

Hata hivyo, alisema wizara ya elimu iko mbioni ili kuhakikisha chuo cha Ufundi Kengeja kinarudi katika hadhi yake ya zamani kwani ndio tegemeo kwa taifa katika masuala ya ufundi.

Mapema Januari mwaka huu, Waziri Nchi katika Afisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Fatma Abdulahabib Fereji wakati akiweka jiewe la msingi jengo la madarasa manne ya skuli hiyo, aliwaahidi kuyapatia ufumbuzi matatizo mbali likiwemo la mabweni na upungufu wa walimu.

No comments:

Post a Comment