Friday, 25 February 2011

Tanzania, UAE kufufua Tume ya Pamoja

Tanzania, UAE kufufua Tume ya Pamoja

Mwandishi Maalum, Dar
Kukutana na ujumbe wa UAE na Balozi wa Brazil

UMOJA wa Falme za Kiarabu (UAE) umesisitiza umuhimu wa kuifufua Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na nchi za ukanda huo.

Hayo yameelezwa jana na Waziri wa Nchi kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu Dk. Reem Ibrahimi Al Hashimy alipokutana na Makamu wa Rais Dk. Mohammed Gharib Bilal, Ikulu jijini Dar es salaam alipokwenda kwa ajili ya kumsalimia.

Dk. Reem alisema kufufuliwa kwa Tume hiyo mapema kutasaidia kukuza na kuendeleza uhusiano wa muda mrefu uliopo kati ya nchi hizo kwa vile maeneo ya ushirikiano yatafahamika na kupewa kipaumbele.

“Naamini Tume ya Pamoja ya Ushirikiano ni chombo muhimu. Tunahitaji kuifufua, mara ya mwisho ilikutana mwaka 1995, ni muda mrefu. Tunahitaji kusaini makubaliano, kama vile makubaliano ya kuzuia ulipaji wa kodi mara mbili kulingana na taratibu za kodi za nchi husika, ni lazima tuwe na Tume ya Pamoja kufanikisha haya,” alisema Waziri huyo.

Akizungumzia uwekezaji Dk. Reem alisema angependa kuorodhesha fursa za uwekezaji zilizoko nchini na kuzichukua kuzipeleka UAE na wale ambao wataonesha nia ya kutaka kuwekeza waweze kuja Tanzania.

Dk. Reem ambaye alikuwa anaongoza ujumbe wa watu wapatao kumi kutoka UAE alikuwa nchini kwa ziara ya kikazi ambapo alifungua jengo jipya la ubalozi wa UAE.

Katika mazungumzo hayo Dk. Bilal alimhakikishia Waziri huyo kuwa serikali ya Tanzania inatambua umuhimu wa Tume hiyo na kwamba mipango iko katika hatua za mwisho za kusaini makubaliano ya kuifufua Tume hiyo.

Kwa upande wa uwekezaji Makamu wa Rais alisema Tanzania inakaribisha wawekezaji kutoka UAE kuwekeza kwenye sekta mbalimbali hususan za kilimo, madini, miundombinu ya barabara, nishati pamoja na mawasiliano.

Wakati huo huo, Dk. Bilal amekutana pia na Balozi wa Brazil nchini, Carlos Soares Luz ambapo wamezungumzia masuala mbalimbali yenye lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Brazil yakiwamo ya michezo, nishati, kilimo na ya jamii kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment