Tuesday 1 February 2011

SERIKALI KUIELIMISHA JAMII ATHARI ZA TABIANCHI

Serikali kuielimisha jamii athari za tabianchi

Na Evelyn Mkokoi, Mtwara
SERIKALI imedhamiria kuelimisha jamii ya kitanzania juu ya athari na namna ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, kupitia wa kwa wadau wa sekta mbali mbali.

Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Mazingira kutoka ofisi ya Makamu wa Rais, Richard Muyungi, alieleza hayo jana katika warsha ya wadau wa kanda ya kusini iliyofanyika mkoani Mtwara.

Muyungi alisema nchi zinaoendelea ikiwemo Tanzania zinakabiliwa na changamoto mbali mbali zitokanazo na mabadiliko ya Tabia nchi ikiwa ni pamoja na mafuriko akitolea mfano mafuriko ya Kilosa.

Aidha alisema kuwa athari nyengine ni ongezeko la magonjwa kama vile malaria zaidi katika maeneo ambayo awali malaria haikuwa tishio kama vile Lushoto, kituro Rungwe na Njombe.

Mkurugenzi huyo alifahamisha kuwa kuna kila sababu ya jamii kuelewa kuhusu mabadiliko ya tabia nchi umuhimu wake na changamoto zake ikiwa ni pamoja na umaskini.

Akifungua warsha hiyo mwakilishi wa Ofisa tawala wa Mkoa wa Mtwara, Smythies Pangisa alisema athari zaidi ya mabadiliko ya tabia nchi katika vizazi vijavyo ni ukosefu wa maji safi, kuongezeka kwa hali ya jangwa katika baadhi ya maeneo na viumbe kutoweka.

Warsha hiyo ya siku mbili iliyoandaliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, imehusisha mada ya mabadiliko ya Tabia nchi na Sera ya Taifa ya Mazingira, sheria ya usimamizi wa mazingira na utekeleazaji wake, imehudhuriwa na wadau mbali mbali wakiwemo maofisa maliasili na mazingira, mahakimu, wadau kutoka katika asasi za kiraia, NGO’s na wanahabari.

No comments:

Post a Comment