Wednesday, 23 February 2011

Mama Mwanamwema asifu kinamama kwa kuichagua CCM

Mama Mwanamwema asifu kinamama kwa kuichagua CCM


Na Mwanajuma Abdi

MKE wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mama Mwanamwema Shein amesema ushindi wa CCM umetokana na ridhaa ya wananchi waliyokikubali chama hicho ili kiwaletee maendeleo.

Hayo aliyasema jana Kilimahewa bondeni, wakati alipokwenda kuwapongeza wananchi na wanaCCM waliokipigia kura chama hicho na kuwawezesha Rais Shein, wabunge, wawakilishi na madiwani kushinda katika uchaguzi uliopita.

Alisema ushindi huo umetokana na ridhaa ya wananchi kukikubali chama hicho kwa kimefanya mambo makubwa ya maendeleo nchini chini ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuanzia awamu ya kwanza.

Mama Mwanamwema aliwahimiza akinamama na akinababa kwamba uchaguzi umekwisha kwa salama na amani na kilichosalia hivi sasa ni kuchapa kazi kwa bidii kwa lengo la kujiletea maendeleo katika sekta za biashara, kilimo na ufugaji.

Aidha alihimiza umoja, mshikamano, utulivu na amani iliyopo nchini iendelee kuwepo, kwa sababu ya kupatikana maendeleo ya haraka, kwani bila ya hayo nchi haiwezi kupiga hatua za haraka za kiuchumi.

Nae Mke wa Makamu wa pili wa Rais, Mama Asha Seif Ali Iddi, aliweka mkazo kwa akinamama kuendeleza kampeni za kukiletea ushindi chama hicho, kwa vile wao wanaushawishi mkubwa katika jamii.

Risala ya wananchi wa Shehia ya Kilimahewa Bondeni, ilisema kwamba walijitokeza kwa wingi katika uchaguzi uliopita, jambo ambalo limesaidia Chama hicho kushinda.

No comments:

Post a Comment