Tuesday 22 February 2011

CCM MJINI MAGHARIBI YAJIANDAA SHEREHE YA USHINDI WA DK. SHEIN

CCM Mjini Magharibi yajiandaa sherehe ushindi wa Dk.Shein

Na Mwantanga Ame

CHAMA cha Mapinduzi Mkoa wa Mjini Magharibi kimeanza shamrashamra za kuadhimisha ushindi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, aliyekuwa Mgombea wa CCM katika nafasi ya Urais.

Shamrashamra hizo zitaanza kwa misafara ya matembezi ya pikipiki yatakayopita katika majimbo yote Mkoani humo kwa siku nne.

Akizungumza na Zanzibar Leo, Katibu wa CCM Mkoa huo, Ramadhani Abdalla Ali, alisema matembezi hayo yanalenga kumpongeza, Dk. Ali Mohammed Shein kwa kupata ushindi kwenye uchaguzi huo.

Aidha, Katibu huyo, alisema sherehe hizo zitakazofikia kilele chake Februari 26, Dk. Shein, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mkutano wa hadhara utakaofanyika uwanja wa Demokrasia Kibandamaiti.

Alisema matembezi hayo yatabeba ujumbe maalum utakaofikishwa kwa wanachama ukihimiza wana CCM kujiandaa na uchaguzi mkuu wa ndani wa chama hicho utakaofanyika mwakani.

Ujumbe mwengine utawataka wanachama kufikiria njia za kuitekeleza Ilani ya CCM kwa miaka mitano ijayo.

Kutokana na shamrashamra hizo, Katibu huyo aliwataka wana CCM katika majimbo ya Mkoa huo, kujitokeza kwa wingi kufanikisha shughuli hiyo na kuhudhuria mkutano wa hadhara.

Wakati huo huo, uongozi wa Mkoa wa Mjini umewapongeza Wawakilishi, Wabunge na Madiwani kwa kufanikisha uchaguzi mkuu.

Kikao hicho kilifanyika katika Afisi ya Chama Mkoa kikiwa chini ya Katibu wa CCM Mkoa wa Mjini Maharibi, Ramadhan Abdalla Ali.

Hata hivyo, Katibu huyo aliwaonya wajumbe hao kuacha kubweteka baada ya kupata ushindi wa kuongoza majimbo na badala yake washiriki katika vikao vitavyokuwa vinaandaliwa na wanachama wao katika majimbo yao.

No comments:

Post a Comment