Sunday 27 February 2011

VIROJA VYAAZA LIGI KUU MJINI

 Viroja vyaanza ligi Mjini

 Mashabiki, wachezaji wachapana, kanuni zakiukwa
Na Mwajuma Juma

MICHEZO miwili ya ligi daraja la pili Wilaya ya Mjini katika viwanja viwili tafauti, imeshinda kumalizika kwa sababu mbalimbali zikiwemo vurugu za mashabiki.

Pambano lililozikutanisha timu za Dynamo na University katika uwanja wa Amaan B, lilivunjika kabla ya wakati baada ya kutokea vurugu baina ya wachezaji na mashabiki.

Tafrani hiyo ilitokea katika dakika ya 79 ambapo hali ya amani ilitoweka na muamuzi Sunday Nhomba, kuamua kuuvunja mchezo huo, huku University ikiongoza kwa magoli 2-0, yaliyofungwa na Omar Mohammed na Ramadhan Rashid.

Na katika mchezo mwengine uliochezwa uwanja wa Jeshini, timu ya Maji Maji iliyokuwa imepangwa kuivaa Vijana, ilifika uwanjani bila kuwa na leseni za wachezaji, huku karatasi ya majina ya wachezaji wake ikionesha majina tafauti na ya wale waliokuwepo uwanjani.

Hata hivyo, mchezo huo ulichezwa bila Maji Maji kutimiza kanuni hiyo, lakini baada ya dakika 45 za kwanza, muamuzi Shaaban Sadik aliuvunja kutokana na timu hiyo kushindwa kuwasilisha vitu hivyo hata baada ya kupewa muda.

Hadi muamuzi anavunja mchuano huo, matokeo yalikuwa sare ya 1-1, ambapo Vijana lilifungiwa goli lake na Machano Masoud, huku Said Mbwana akipachika lile la Maji Maji.

Kuhusiana na kasoro hizo, Katibu Msaidizi wa ZFA Wilaya ya Mjini Omar Mohammed, alisema hatima za matokeo ya mechi hizo, itajulikana baada ya kupata ripoti za waamuzi na makamisaa.

Matokeo ya mechi nyengine za ligi hiyo mwishoni mwa wiki, yalikuwa FC Roma 4, Mwembenjugu 0, Zainab Bottlers 1, Star Kids 1, Super Sports 3, Magomeni 2, Jang'ombe Boys 2, Dangers 1, Spirit 2, Union Rangers 2.

Aidha Maruhubi iliifunga Kundemba 3-1, Red Stars ikang'ara mbele ya El Hilal kwa ushindi wa magoli 4-1, na Kombora ikairipua Enugu mabao 2-0.

No comments:

Post a Comment