Wednesday, 23 February 2011

PBZ YALIPIGA TAFU BONAZA LA WANAHABARI

 PBZ yalipiga ‘tafu’ Bonanza la wanahabari

Na Mwantanga Ame


UONGOZI wa Shirika la Magazeti ya Serikali Zanzibar, umepokea msaada wa fulana maalumu kutoka Benki ya Watu wa Zanzibar kwa ajili ya kufaniksha Bonanza la kimichezo litakalojumuisha wafanyakazi wa vyombo vya habari hapa nchini.

Katika hafla ya makabidhiano hayo iliyofanyika jana kwenye Makao Makuu ya benki hiyo Darajani, Mkurugenzi wa benki hiyo Juma Amour alisema taasisi yake itaendelea kutoa misaada kwa huduma za kijamii ikiwemo michezo kwa kuthamini mchango wa wananchi katika kuimarisha huduma za benki hiyo.

Mkurugenzi huyo alisema, benki hiyo ni ya wananchi wa Zanzibar na ili huduma zake ziimarike, misaada yake kwa jamii ni muhimu na pia ni sehemu ya kujitangaza kibiashara.

Aidha alifahamisha kuwa msaada wa PBZ kwa ajili ya Bonanza unalenga kuthamini mchango wa vyombo vya habari katika kuipatia taaluma jamii juu ya mambo mbali mbali.

Mkurugenzi huyo aliahidi kuendelea kushirikiana na vyombo vya habari ikiwa ni hatua itayokuza uhusiano kati yao na jamii.

Naye Mhariri Mtendaji wa Shirika la Magazeti ya Serikali Abdallah Mohammed Juma, akitoa shukrani, alisema msaada wa benki hiyo ni faraja kwa taasisi yake, na kwamba kukubali kudhamini Bonanza hilo kutasaidia kuleta ufanisi.

Alisema Shirika lake litahakikisha ushirikiano ulioanzishwa ambao umeonesha wazi nia njema ya kujenga uhusiano, unadumishwa kwa manufaa ya taasisi yake na zile za kifedha.

Bonanza hilo linalohusisha aina mbalimbali za michezo na burudani, limepangwa kufanyika Februari 26, mwaka huu katika viwanja vya Maisara ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Bihindi Hamad Khamis.

No comments:

Post a Comment