Wednesday, 23 February 2011

Ongezeko la baa lachangia utumiaji dawa za kulevya

Ongezeko la baa lachangia utumiaji dawa za kulevya

Na Mwanajuma Abdi

WANANCHI wa vijiji vya Paje, Bwejuu, Muyuni na Makunduchi wamesema kuzagaa kwa baa mitaani kunachangia ongezeko la watumiaji wa dawa za kulevya na kuchangia maambukizi ya mapya ya UKIMWI.

Kauli hizo walizitoa jana, katika majadiliano ya pamoja yaliyoandaliwa na Jumuiya ya ZAYEDESA chini ya ufadhili wa Shirika la ICAP na CDC kupitia watu wa Marekani, yaliyofanyika katika skuli ya Paje Mkoa wa Kusini Unguja, yaliyowashirikisha masheha, walimu na maofisa wa Wilaya na waelimishaji rika.

Walisema katika vijiji hivyo, kuna baadhi ya baa zinachangia kuharibu maadili ya vijana kutokana na kujaa ushawishi wa utumiaji dawa za kulevya, jambo ambalo linalolitilia nguvui uwezekano wa maambukizi mapya

Baadhi ya baa katika kijiji hicho zimejenga tabia ya kingza magari yakiwa na wanawake wanaodaiwa kuwa na mavazi nusu uchi

Katibu wa Sheha wa Michamvi, Abeid Juuyahaji, alishauri Serikali kutofumbia macho baa zilizoibuka kiholela, ambazo hazimo katika mahoteli makubwa ya kitalii ziondoshwe katika ukanda huo.

Alisema wananchi wamejaribu kuchukua hatua kadha kutaka kuziondosha lakini wamiliki wake huwatisha wananchi kwa jeuri zao za fedha.

Mwananchi mwengine wa kijiji hicho, Issa Juma alishauri maduka yanayokodisha kanda yawe yakikaguliwa ili kuepusha kukodishwa vijana filamu zinazokiuka maadili na mila za kizanzibari kwani kufanya hivyo kutapunguza matatizo ya UKIMWI na dawa za kulevya kwa vile kuna baaadhi ya michezo inachangia.

Naye Mwalimu Salama Jecha Zidi, aliwashauri wazazi washirikiane katika kupiga vita masuala hayo, ambapo kama katika kijiji wapo vijana watatu au sita wawekee mikatati ya kuwabadilisha tabia, wanaweza kubadilika katika kipindi kifupi.

Mapema Sihaba Saadat kutoka Tume ya UKIMWI Zanzibar alisema kundi kubwa la watumiaji wa dawa za kulevya ni vijana, ambapo waathirika wakuu ni wanaume, na kwa maradhi ya UKIMWI waathirika wakubwa ni wanawake kulingana na hali ya maumbile.

Akifungua mjadala huo, Katibu wa ZAYEDESA, Lucy Majaliwa alisema mjadala huo unalengo la kuwasaidia vijana waliojitumbukiza katika matatizo hayo kutafuta njia za kuweza kuwaokoa na janga hilo.

No comments:

Post a Comment