Haki za wenye ulemavu zilindwe
Na Raya Hamad, OMKR
OFISA Utetezi kutoka Idara ya Watu wenye Ulemavu, Idrissa Khamis Juma amesema jamii inayo haki ya kuelewa na kufahamu mahitaji ya msingi ya watu wenye ulemavu.
Ofisa huyo alisema kutokana na hali hiyo si busara walemavu kuendelea kunyanyaswa sambamba na kunyimwa haki zao kutokana na maumbile yao yalivyo.
Ofisa huyo alieleza hayo kijiji cha Pwanimchangani alipofanya ziara ya uhamasishaji kwa Watu wenye Ulemavu.
Akitoa ufafanuzi kuhusu haki za watu wenye Ulemavu, alisema Watu wenye Ulemavu hawana budi kufahamu na kuielewa Sera, Sheria ya Watu wenye Ulemavu na Mkataba wa Kimataifa.
Idrissa alisema kueleweka kwa haki hizo za msingi kwa Watu wenye Ulemavu kutasaidia kuondokana na mtazamo wa kuwa walemavu daima ni watu wa kusaidiwa na badala yake watafahamu kuwa wanazodai ni haki zao na sio msaada ambao wanastahiki kupewa kama walivyo wengine wowote katika nchi.
Kuhusu suala la Elimu, aliwataka Watu Walemavu kuendelea kutafuta elimu na kupatiwa elimu “Ingawa Serikali imeanzisha kitengo maalum cha elimu mwaka 1992 bado watu wenye ulemavu walio wengi wamekoseshwa haki hii kutokana na ulemavu wao kwa kufuata skuli masafa marefu na kukosa visaidizi, wazazi na walezi kuwaficha majumbani ni miongoni mwa sababu zinazopelekea kukosa rasilimali hii muhimu kwa maisha”, alisisistiza Idrissa.
Aidha Idrissa ameiasa jamii kuacha kutumia maneno yenye kudhalilisha Watu Wenye Ulemavu na kutolea mfano wa maneno hayo ikiwa ni pamoja na mtu asiyeona kumuita kipofu ,Mlemavu wa Akili kumuita Chizi au Akili taahira, Albino kumuita Zeruzeru au Dili nk.
Wakichangia mada washiriki wa mkutano huo wamesema kuwa tatizo kubwa walilonalo katika kijiji chao ni kutopewa kipaumbele hasa wakati wanapopeleka maombi ya kazi hasa mahotelini “Kazi nyengine huwa hazitaki kisomo kama kutupa taka ama kuzoa takataka za ufukweni lakini tunapokwenda kuomba huwa hatupewi kwa sababu ya Ulemavu tulionao”alisema Madai Haji.
Madai Haji Silima ni Mlemavu wa macho na mtoto wake pia ni kiziwi na mwenye matatizo ya macho ambae ameacha kusoma darasa la 7 mwaka 2010 kutokana na matatizo aliyonayo na hivyo amebakia nyumbani akiwa hana la kufanya.
Nae Hamad Khamis aliiomba Serikali kuwasaidia Watu wenye Ulemavu kama wanavyosaidiwa Wazee wasiojiweza pamoja na Idara ya Watu Wenye Ulemavu kuendelea kutoa Elimu juu ya uelewa wa haki za Watu wenye Ulemavu.
Idara ya Watu wenye Ulemavu imeandaa utaratibu maalum wa kuwahamasisha Watu wenye Ulemavu na wasio na Ulemavu kuanzia Mjijni hadi Vijijini kwa Unguja na Pemba.
Tuesday, 22 February 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment