Sunday, 27 February 2011

WANAFUNZI WATAHADHARISHWA KUEPUKA MIGOMO

Wanafunzi watahadharishwa kuepuka migomo

Na Ligwa Paulin

WANAFUNZI wanaofaulu kujiunga na vyuo vikuu nchini wametakiwa kujiepusha na migomo na maandamano yasiyo na tija na badala yake kujihusisha na kilichowapeleka vyuoni kwa manufaa yao na taifa.

Tahadhari hiyo imetolewa mwishoni mwa wiki katika sekondari ya Nyuki Mwanakwerekwe na ofisa mwandamizi wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania Kanali Kidunda Ahmed Mangiri kwenye mahafali ya pili ya kumaliza kidato cha sita skulini hapo.

Alisema baadhi ya Vyuo Vikuu, Tanzania vimekuwa vikikumbwa na migomo au maandamano ambayo kama mwanafunzi hayamsaidii na badala yake yanaweza kusababisha madhara.

Kanali Mangiri ambae pia ni Kamanda wa kikosi cha Jeshi kambi ya Mtoni Unguja, alisema hata kama baadhi ya madai au kero zao ni za msingi lakini njia wanazotumia kuwakilisha matatizo yao sio sahihi.

Alisema wanafunzi hawana budi kudai haki zao kwa kufuata taratibu za chuo husika na kuzingatia sheria za nchi.

Kanali Mangiri ambaye alikuwa mgeni rasmi, alisema anashangazwa na hatua za wanafunzi kama hao ambao wanakuwa na nidhamu wawapo sekondari na nyumbani kwao lakini wabadilike wanapoingia vyuoni.

"Hiyo ni dalili ya kurubuniwa na wenzao wasiolelewa kwa maadili mema majumbani kwao sambamba na sekondari wanazotoka pia wasiowatakia maendeleo mazuri wenzao," alidokeza.

Mapema mkuu wa shule hiyo inayomilikiwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania, Meja Khamis Lusuna akimkaribisha mgeni huyo, alisema mahafali ya mwaka huu kuna wahitimu 22 kati yao wananane wanawake, wakati mwaka jana wahitumu walikuwa 30 ambapo 20 kati yao walifaulu kujiunga na vyuo vikuu mbalimbali nchini.

No comments:

Post a Comment