Tuesday 1 February 2011

TANZANIA YAJUMUISHWA KUSAKA AMANI IVORY COAST.

Tanzania yajumuishwa kusaka amani Ivory Coast



Rais Kikwete azindua muongo vita dhidi ya malaria
Na Mwandishi Maalum, Addis-Ababa

TANZANIA imeteuliwa kuwa moja ya nchi tano zitakazounda kamati ya Umoja wa Afrika katika kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa kisiasa unaoendelea nchini Ivory Coast, kati ya Rais anayemaliza muda wake Laurent Gbagbo na Alassane Outtara.

Nchi nyengine katika kamati hiyo ni Chad, Mauritania, Nigeria na Afrika Kusini, ambazo zitaungana na Burkina Faso ambayo tayari inashughulikia mgogoro huo.

Kamati hiyo imefanya mkutano wake wa kwanza juzi mjini Addis Ababa ambapo imekubaliwa kuwa kila nchi itachagua mwakilishi wake katika kamati ndogo ya wataalamu hapo kesho, ambao watakwenda nchini Ivory Coast kuangalia na kutathmini hali ilivyo.

Kamati ya wataalamu watatakiwa kutoa taarifa na ushauri kwa viongozi ambao hatimaye watakwenda Ivory Coast na kukutana na viongozi hao wawili wanaogombea madaraka.

Wakati huo huo, Rais wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete amesema mwaka 2011 ni mwanzo wa muongo wa vita dhidi ya malaria barani Afrika.

Rais Kikwete, ambaye ni Mwenyekiti wa Mshikamano wa Viongozi wa Afrika Dhidi ya Malaria (African Leaders Malaria Alliance-ALMA), alisema hayo wakati akifungua kikao cha viongozi wa nchi 35 za Afrika zinazounda mshikamano wa kupambana na malaria barani Afrika.

“Mwaka wa 2011 ni mwanzo wa muongo mpya katika Afrika dhidi ya malaria, pia unaashiria mstari wa mwisho katika kukaribia mwisho wa juhudi hizi katika kufuta vifo vinavyotokana na malaria kuelekea mwaka 2015”, Rais Kikwete aliueleza mkutano huo.

Amesema hatua muhimu iliyopigwa na nchi za Afrika katika kufikia malengo ya milenia ambayo yamewekwa na nchi hizi kama wanachama wa familia ya Umoja wa Mataifa na kubainisha kuwa kulingana na ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya mwaka 2010, vifo vinavyotokana na malaria vimepungua barani Afrika.

Katika kikao hicho nchi nne zimefuzu na kupokea tunzo ya kwanza ya ubora na umakini katika juhudi za kupambana na malaria zikiwemo Tanzania, Guinea, Kenya na Uganda.

Juhudi zilizofanywa na nchi hizi ni pamoja na kukuza uhusiano na kuharakisha upatikanaji wa fedha, kudhibiti na kukuza matumizi ya kinga ya malaria, mfano ikiwemo matumizi ya vyandarua, kufuta na kusitisha utengenezaji, usambazaji na matumizi ya dawa aina ya Artemisinin, kuondosha kodi na kuunga mkono utengenezaji na uzalishaji wa dawa za malaria barani Afrika.

Rais Kikwete alipokea tunzo hiyo katika kikao hicho na kushuhudiwa na nchi wanachama akiwemo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon, mwenyeji wa Mkutano wa Viongozi wa Afrika wanaohudhuria kikao jijini Addis Ababa Waziri Mkuu Meles Zenawi viongozi wa mashirika ya kimataifa na nchi rafiki.

Kikao hicho kimemchagua Rais wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf kuwa Makamu Mwenyekiti wa ALMA.

No comments:

Post a Comment