Friday 25 February 2011

Hakuna mwananchi atakaekufa njaa-Balozi Seif

Hakuna mwananchi atakaekufa njaa-Balozi Seif

 Awataka wakulima kuwa wastahamilivu
Na Mwantanga Ame


HEKTA 50 za mpunga zimeharibika baada ya kukumbwa na kiangazi katika Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Hali hiyo imeyaathiri mabonde ya mpunga ya Kilombero, Muembempunga, Kibokwa na Machekechuni.
Mengi ya mabonde yamekauka huku mpunga uliopandwa ukishindwa kustawi huku migomba, mihogo nayo ikiwa imeungua kutokana na kiangazi kinachoendelea.

Akizungumza na wakulima, Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi, alisema serikali inasikitishwa na hali hiyo na kuwataka wakulima kuwa wastahamilivu wakati huu mvua ya masikika ikitarajiwa kunyesha mapema mwezi ujao.

Balozi Seif alisema serikali itahakikisha hakuna mwananchi ataekufa kwa njaa na itahakikisha wananchi wanapatiwa chakula cha dharura.

Alisema hali hiyo imesababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa duniani, ambapo tayari athari za aina hiyo zimeonekana kujitokeza kwa upande wa Tanzania Bara na Pemba.

Aidha alisema serikali inajali hasara iliyowapata wakulima katika kutayarisha mashamba yao na itachukua hatua za kuwalimia mashamba yao bure mara mvua zitakapoanza kunyesha.

“Hali sio nzuri inaitia hasara serikali kwani mazao yatachelewa na itatulazimu kununua chakula kutoka nje jambo ambalo litakuwa gumu kwani duniani kumejaa hali ya machafuko, lakini tunakuombeni mstahamili na tuombe mvua inyeshe,” alisema Balozi Seif.

Tatizo la ukosefu wa mvua pia limeonekana kusababisha ukosefu wa uzalishaji wa mazao ya chakula katika wilaya ya Micheweni kisiwani Pemba.

Maafisa wa Kilimo katika mabonde hayo wamesema hali huenda ikawa mbaya kuweza kupata mazao ikiwa msimu wa masikika utamalizika bila mvua kunyesha.

Hekta ambazo zimelimwa katika bonde la Mayungi ni 50 lakini tayari hekta 10 zimeungua kwa jua huku zilizobakia zikiwa zimeanza kutoa mpunga ambao hautaweza kustawi.

Walisema hali ni mbaya zaidi katika mabonde ya mpunga ya Mkoa wa Kaskazini huku upande wa Kusini ukiwa na hali inayoridhisha kwa baadhi ya mabonde likiwemo Cheju na Mtende ambapo asilimia 47 ya mpunga umeweza kuota vizuri.

Katika Bonde la Kibokwa, hali pia sio nzuri ambapo ekari 6,339 zilichimbwa huku zilizoburugwa ni 5,3505 na zilizolimwa ni ekari 3,600.75 lakini zilizoharibika ni ekari 795.5.

Zanzibar Leo imeshuhudia baadhi ya mito ikiwa imekauka katika mabonde hayo na kuathiri mashamba ya wakulima wa ushirika wa mboga mboga wa Ukweli ni Vitendo.

Mwenyekiti wa ushirika huo, Tatu Khamis alisema mto waliokuwa wakiutegemea kumwagilia kwa sasa umepungua maji.

Katibu Mkuu wa Wizara Kilimo na Misitu, Afani Othman Maalim, alisema Wizara yake imeunda Kamati maalum kwa ajili ya kufuatailia suala hilo na huenda wiki ijayo ikawa na ripoti kamili juu ya kiasi gani cha athari kilichotokea.

Alisema maeneo ambayo Kamati hiyo inayaangalia ni pamoja na kutathmini maeneo ambayo yatahitaji kuburugwa tena, na athari zilizowapata wakulima ili kuona vipi serikali itaweza kuwasaidia.

No comments:

Post a Comment