Tuesday, 22 February 2011

IRAN KUJENGA CHUO CHA AMALI

Iran kujenga Chuo cha Amali



Na Haji Chapa, MUM

KATIKA kuendeleza mahusiano mazuri ya kidiplomasia serikali ya Jamuhuri ya watu wa Iran, ina mpango wa kujenga chuo cha mafunzo ya amali hapa Zanzibar.

Balozi wa Iran nchini, Mohsen Movahhedi Ghomi alieleza hayo alipofanya mazungumzo na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Ramadhan Abdalla Shaaban huko ofisini kwake Mazizini nje kidogo ya mji wa Zanzibar.

Balozi huyo akiwa ameambatana na ujumbe wa watu watatu, alisema kutokana na mahusiano mazuri yaliyopo baina ya Iran na Zanzibar, nchi hiyo imetenga dola 500,000 za ujenzi wa Chuo hicho.

Mbali na hayo Balozi Ghomi, alisema nchi hiyo pia itaendelea kushirikiana na Zanzibr katika kukuza nyanja ya utamaduni ambapo katika hilo itaisadia Zanzibar katika kuikuza sekta ya Utalii.

Katika kuimarisha tamaduni za nchi mbili ni faraja kubwa kuwekeza katika suala la elimu kwani katika hilo vile vile wameazimia kuanzisha ofisi itakayohusika na suala la elimu na kuweka mashirikiano mazuri na taasisi zisizo za kiserikali (NGOs) alieleza hayo.

Aidha Balozi huyo alisema Zanzibar sio nchi ya kubezwa kutokana na asili yake na umuhimu wake wa kitamaduni kwani unafahamika nchi nyingi duniani kwa kutaja mfano wa mwaka kogwa.

Naye Waziri Ramadhani aliishukuru Jamuhuri ya watu wa Iran kwa uamuzi wao huo wa kutaka kuwekeza katika suala la elimu kwani utaimarisha mahusiano yao ya kitamaduni na kielimu.

Aidha aliiomba Iran kuwekeza zaidi katika sekta hiyo ya elimu na utamaduni na kutumia fursa ya amani na utulivu uliopo Zanzibar kuimarisha mashirikiano.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu Abdalla Mzee Abdalla, aliyaelezea mashirikiano ya Iran na Zanzibar katika sekta ya elimu ni ya muda mrefu.

Alisisitiza juu ya nchi hiyo kufanya uthibitisho wa ujenzi wa kituo hicho cha Mafunzo ya Amali ikiwa ni kupata barua rasmi.

No comments:

Post a Comment