Tuesday 22 February 2011

WIZARA ELIMU KUKAMILISHA UJENZI WA MADARASA

Wizara Elimu kukamilisha ujenzi wa madarasa

Na Khamisuu Abdallah

NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Abdulla Mzee Abdulla, amesema kutokana na kufaulu kwa kiwango kikubwa wanafunzi mwaka huu Serikali inafanya jitihada za kukamilisha na kujenga madarasa katika Skuli mbali mbali za Unguja na Pemba.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, ofisini kwake Mazizini, Naibu Katibu Mkuu huyo alisema kutokana na wingi wa wanafunzi waliofaulu, Serikali ya awamu ya saba imeshakamilisha ujenzi wa madarasa 150 katika Skuli mbali mbali zilizopo nchini.

Alieleza kuwa katika kukamilisha ujenzi huo, Serikali ina mpango wa kujenga madarasa 250 kwa kupitia wafadhili ambao ni kutoka nchini Sweden na Ubalozi wa Marekani ambao ni wafadhili waliojitolea kukamilisha ujenzi huo.

Abdulla, alisema hivi sasa Serikali imekuwa ikifanya jitihada za kujenga Skuli mbali mbali ambazo zitakidhi mahitaji katika vijiji mbali mbali ili kuweza kutoa elimu kwa watoto wote hapa nchini.

Alisema katika kulitatua tatizo hilo, Serikali ipo katika mchakato wa kujenga Skuli mbali mbali za 21 kwa Unguja na Pemba,ikiwemo Dimani,Shamiani pamoja na Wete ambazo wanafunzi watatumia teknolojia ya kisasa ikiwemo kutumia kompyuta pamoja na intaneti ili kuweza kwenda na wakati.

"Serikali ya awamu ya saba tunataka wanafunzi wasome pazuri, wakae pazuri ili wanafunzi waweze kufaulu vizuri kwa kutumia teknolojia itakayokuwepo katika maskuli mbalimbali,"alieleza.

Aidha aliwataka wananchi kujitoa nguvu zao katika ujenzi wa maskuli ili Serikali iweze kuwaunga mkono kuweza kukamilisha ujenzi huo ili kuboresha elimu nchini.

Aidha amewapongeza Skuli ya msingi ya Mtopepo "B" pamoja na Skuli ya Mtopepo kwa kupasisha wanafunzi wengi kila mwaka, sambamba na kuwataka wazazi kuwahimiza watoto wao kujitahidi katika masomo yao.

No comments:

Post a Comment