Sunday, 27 February 2011

Wakulima wa mpunga wasifia maandalizi msimu huu

Wakulima wa mpunga wasifia maandalizi msimu huu

Na Mwantanga Ame

WAKULIMA nchini wamejitayarisha vizuri kwa kilimo cha msimu ujao endapo mvua zitanyesha kwa wakati

Wakulima hao waliyasema hayo wakati Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi, alipofanya ziara kuangalia hali ya jua kali na ukame uliosababisha mazao mbali mbali kufa na kilimo cha mpunga kuzorota.

Wakulima wa mabonde ya Kilombero, Muembe Mpunga, Kibokwa na Mchekeni, walieleza kuwa walijiandaa na kufanikiwa kupanda mpunga mapema lakini hali ya kiangazi imesababisha mpunga kufifia na mazao mengine ya kilimo cha juu kufa.

Mkulima Ukasha Abdi Ukasha, akizungumza kwa niaba ya wakulima wenzake alisema mwaka huu maandalizi ya kutayarisha mabonde ya mpunga yalikuwa mazuri ingawa kilimo chenyewe cha mpunga kimezorota kutokana na jua kali.

“Kwa hili tunaishukuru Wizara ya Kilimo, kwa kweli imetulimia kwa wakati na imetuburugia kwa wakati ila tuu mvua ndio imetukimbia lakini kama itakuja hapa tungepata mpunga mwingi usiowahi kutokea miaka yote” alisema mkulima huyo.

Mkulima huyo alisema tatizo kubwa ambalo wanakabiliana nalo hivi sasa ni kukosekana kwa mvua jambo ambalo tayari linawapa mashaka ya kuweza kufikia malengo waliyokusudia.

Waziri wa Wizara ya Kilimo na Misitu, Mansoor Yussuf Himid, alisema hekta 30,000 hadi mwezi huu zilishaburugwa na kupandwa mpunga.

Alisema kati ya hekta hizo kwa upande wa Pemba ni 16,000 na Unguja ni hekta 14, 000 ikiwa ni sawa na asilimia 75 ya malengo.

Wakulima waliahidi kutumia mbolea na pembejeo nyengine ili kwa nia ya kuongeza uzalishaji wa mazao.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Afani Othman Maalim, akizungumzia suala la uzalishaji mpunga, alisema endapo wakulima watatumia fursa ziliopo na kujishajiisha wataweza kuvuka malengo.

No comments:

Post a Comment