Tuesday 1 February 2011

BALOZI SEIF ; SMZ YAJIDHATITI KUONDOSHA UHABA WA MADAWATI.

Balozi Seif: SMZ yajidhatiti kuondosha uhaba wa madawati

Na Mwantanga Ame

MBUNGE wa Jimbo la Kitope, Balozi Seif Ali Iddi amekabidhi madawati 100 kwa wanafunzi wa Skuli ya Kitope, Kilombero na Fujoni ikiwa ni hatua ya kutimiza ahadi yake kwa wananchi Jimbo hilo.

Balozi Iddi ambaye pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, alikabidhi madawati hayo jana katika ziara aliyoifanya katika skuli hizo kwa nyakati tofauti ambapo pia alikabidhi shilingi milioni moja kwa Skuli ya Kitope kwa ajili ya kuwezesha kumaliziwa kwa darasa linalotarajiwa kutumika kwa shughuli za maabara.

Akizungumza na wananchi wa Jimbo hilo, Mbunge huyo alisema kuwa viongozi wa Jimbo hilo wamedhamiria kuona suala la watoto kuandika wakiwa wamepakata mabuku yao katika mapaja linaondolewa kwa vile hawawezi kuona tatizo hilo linashindwa kupatiwa ufumbuzi.

Alisema serikali hivi sasa imo katika mkakati mkubwa wa kupambana na tatizo la ukosefu wa madawati katika skuli zake za Unguja na Pemba, ambapo inahitaji kupata vikalio 30,000.

Alifahamisha kuwa katika kuitekeleza azma hiyo serikali inajiandaa kutoa tamko litalowashurutisha Wabunge wa Jamhuri ya Muungano kuchangia kuondoa matatizo ya aina hiyo katika majimbo yao kupitia fedha za mfuko wa majimbo.

Alisema hatua iliyofikiwa katika Jimbo hilo hivi sasa ni ya kuridhisha kwa baadhi ya skuli jambo ambalo linatarajiwa wanafunzi wa skuli hizo kufanya vizuri katika masomo yao.

Akizungumzia matatizo ya baadhi ya walimu wanaojitolea kuweza kusaidiwa kupata posho la kuwakimu, alisema ataendelea kuliangalia suala hilo kwa kufuata utaratibu uliowahi kutumika hapo awali kwa kuwalipa walimu hao.

Aidha Mbunge huyo aliwataka walimu ambao waliomba kupatiwa vyombo vya moto kwa njia ya mkopo alisema suala hilo tayari Wizara ya Elimu imekubali kuwapatia mikopo hiyo kupitia SACCOS.

Aidha madai ya ukosefu wa maji kutoka kwa wanachi wa eneo la Kirombero na Upenja, alisema tayari hatua za awali imeshazichukua za kutafuta vifaa ambavyo walitakiwa na mamlaka ya maji kuwa navyo na kinachosubiriwa sasa ni shughuli za kitaalamu kufanyika ili kupata huduma hiyo.

Mapema Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Ramadhan Abdalla Shaaban, akitoa shukrani zake kwa Mbunge huyo alisema serikali imefarajika kuona Mbunge na Mwakilishi wa Jimbo hilo Makame Mshimba wameweza kuanza kutoa misaada hiyo kwa vile ni moja ya mpango mkubwa unaokusudiwa kutekelezwa.

Alisema tatizo la madawati katika maskuli ya Unguja na Pemba hivi sasa ni kubwa na hivi sasa serikali inajiandaa kutekeleza mradi mkubwa kupitia wafadhili, kuchongesha madawati yatayotosheleza kwa skuli zilizopo pamoja na kumaliza mabanda ya skuli.

Waziri huyo alisema kutokana na mchango ulioanza kutolewa na Mbunge huyo Wizara hiyo itahakikisha inalipatia Jimbo hilo madawati 135 ikiwa ni hatua ya kwanza na kuwataka wanafunzi wa skuli hizo kuanza kujiandaa na matumizi ya kutumia mitandao.

Waziri huyo alisema mpango wa serikali wa kuanza matumizi ya mitandaao kwa wanafunzi wa darasa la kwanza unatarajiwa kuanza kufanya kazi mwezi huu, ambapo kila mwanafunzi atakuwa na kompyuta yake kauli ambayo ilishangiriwa na wanafunzi hao.

Nae Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu Abdalla Mzee alisema serikali imekuwa ikitumia shilingi milioni 200 kwa mwaka kwa ajili ya kununulia madawati ambapo huweza kupata madawati 1,200 ambapo skuli zinazohitaji madawati hayo ni 450.

Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Vuai Ali Vuia, alisema uhaba wa vikalio katika skuli za Mkoa huo ni mkubwa lakini inafurahisha kuona uongozi wa Jimbo la Kitope umekuwa ukipambana nalo na kuwataka viongozi wa majimbo mengine kuiga mfano huo.

No comments:

Post a Comment