Sunday, 27 February 2011

Upigaji dawa Kaskazini wafanikiwa

Upigaji dawa Kaskazini wafanikiwa

Na Ismail Mwinyi

MDHAMINI Mkuu wa Kitengo cha Upigaji Dawa ya Malaria Majumbani, wilaya ya Kaskazini ‘B’, Nassor Said Nassor, amesema zoezi la upigaji dawa kwa wilaya hiyo linaendelea vizuri kutokana na wananchi kutoa ushirikiano wa karibu na kitengo hicho.

Alisema kwa vile wananchi wanafahamu umuhimu ya upigaji dawa majumbani kumeweza kuwarahisishia kwa asilimia kubwa kuliendesha vizuri zoezi hilo.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Mdhamini huyo, alisema kutokana na ushirikiano walioneshwa na wananchi wa Wilaya hiyo ni kwamba zoezi hilo limekwenda vizuri ambapo shehia 26 kati ya Shehia 29 za Wilaya hiyo ziliweza kupigwa dawa.

Nassor, alieleza kuwa nyumba 10,165 zimefanikiwa kupiga dawa kati ya nyumba 10,370 zilizopo katika Wilaya hiyo.

Alisema kuwa hivi sasa ugonjwa wa Malaria hapa nchini umeweza kupungua kwa asilimia kubwa kutokana na ushirikiano wa karibu uliooneshwa kati ya wananchi na Wizara ya Afya.

Alieleza kuwa pamoja na kufanikiwa kiasi hicho lakini pia walipambana na vikwazo kadhaa ikiwemo visingizio mbali mbali ili nyumba zao zisipigwe dawa.

Alisema kuwa wananchi wengi wao walikuwa wakidang’anya kwa kudai nyumba zao zinawagonjwa hivyo hazifai kupigiwa dawa ya kuua mbu wa Malaria.

“Watu hawataki kupigiwa dawa ndio maana wanadai kuwa wanawagonjwa dani kutokana na taratibu zetu hatuwezi kupiga dawa nyumba hizo kutokana na kuwepo kwa wangonjwa,hicho ndio kisingizio chao kikubwa,”alisema.

Zoezi la upigaji dawa majumbani kupunguza Malaria katika Wilaya ya Kaskazini B, ilianza Januari 24 mwaka huu na limemalizika Februari 26.

No comments:

Post a Comment