Walimu 3,000 maandalizi kupatiwa mafunzo
Juma Khamis
KIASI cha walimu 3,000 wa maandalizi Unguja na Pemba watapatiwa mafunzo ya kujifunza kwa njia ya redio na video kupitia mradi wa ZTUR.
Mafunzo hayo yatawasaidia walimu wa maandalizi kuweza kubuni njia mpya za kuwafundisha wanafunzi ikiwa ni njia moya ya kuimarisha kiwango chao cha ufahamu na kupiga jeki maendeleo ya sekta ya elimu nchini.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya programu zilizotayarishwa na ZTUR, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Ramadhan Abdulla Shaaban, alisema mradi wa ZTUR umeweka mazingira mazuri yatakayompa mwalimu mbinu tafauti za kutayarisha vipindi kwa vitendo vitakavyochangamsha ubongo wa mtoto na kuongeza ari ya kujifunza zaidi.
Aidha alisema mradi huo umekuja wakati muafaka kwa kuasaidia azma ya serikali ya kutekeleza sera ya elimu ya mwaka 2006 ambayo inawataka watoto wote walio na umri wa miaka minne kuanza skuli za maandalizi kabla ya kujiunga na skuli za msingi.
Alisema mafunzo hayo kwa walimu yatatolea kwa kusikiliza redio na kufanya mazoezi pamoja na semina katika vituo vya walimu na yanatarajiwa kuchukua muda wa hadi miaka miaka miwili na nusu, ambapo wahitimu watatunukiwa vyeti baada ya kumaliza mafunzo.
Mapema afisa kutoka Serikali ya Marekani, Robert Scott alisema mradi wa ZTUR umepata mafanikio makubwa tokea kuanzishwa na umekidhi malengo ya kuanzishwa kwake kwa kuzalisha wakufunzi ambao wataweza kuwasomesha walimu wengine wa skuli za maandalizi.
Mradi wa ZTUR umesaidia kutayarisha mafunzo ya walimu kwa njia ya elimu kwa redio na video na njia hii inatarajiwa kuwafikia walimu wengi zaidi katika kipindi kifupi.
Pia mradi wa ZTUR umetayarisha vipindi 20 vya redio vya Chezesha Ufundishe vinavyojumuisha Kiswahili, hesababu pamoja na sayansi, ambapo walimu wa maandalizi watasikiliza vipindi hivyo kupata mbinu za ufundishaji na wakati huo huo wakitayarisha masomo ya kufundisha watoto katika skuli zao.
Aidha ZTUR imetayarisha vitabu mbali mbali vya muongozo ambavyo vimepelekwa skuli zote za Unguja na Pemba na vituo vya walimu, ambapo kiasia cha vitabu 6,000 vimechapishwa, ambapo skuli zote zinaweza kusikiliza vipindi vya redio vya Chezesha Ufundishe na Tucheze Tujifunze kwa kutumia redio.
Mradi ya ZTUR uneandeshwa chini ya ufadhili wa Shirika ka Misaada la Marekani (USAID), Serikali pamoja na Shirika la Elimu la EDC.
Wednesday, 23 February 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment