Wednesday, 23 February 2011

Kasi ya maendeleo ya kilimo Z’bar yawaridhisha wafadhili

Kasi ya maendeleo ya kilimo Z’bar yawaridhisha wafadhili


Na Juma Mohammed, Maelezo

SHIRIKA la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa(FAO) limeridhishwa na kasi ya maendeleo ya kilimo visiwani Zanzibar na umakini wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Akizungumza na uongozi wa Wizara ya Kilimo na Maliasili, Mwakilishi Mkazi wa FAO, Louise Setshwaelo amesema hajaona Serikali inayokwenda kwa kasi kama SMZ katika kuendeleza kilimo na wakulima.

“FAO imefurahishwa sana na Zanzibar…sijaona Serikali inayokwenda kwa kasi kama hii ya SMZ, kama nitaondoka leo basi nitajivunia mafanikio hayo, inatia moyo sana na hongereni” Alisema Louise.

Mwakilishi Mkazi huyo alisema umakini wa Wizara ya Kilimo na Maliasili katika kuendeleza sekta ya kilimo ni wa kupigiwa mfano hasa katika kuwajengea uwezo wakulima katika utafutaji wa masoko na uzalishaji bora wenye kuzingatia maelekezo ya watalaam wa kilimo.

Alisema FAO itatoa kila aina ya msukomo kuisaidia Zanzibar kufikia malengo yake ikiwa pamoja na kushawishi Washirika wa maendeleo kuendelea kuisaidia hasa katika uhakika wa chakula na lishe.

Akizungumza katika mkutano huo, Waziri wa Kilimo na Maliasili, Mansoor Yussuf Himid alisema Serikali itawasilisha katika Baraza la Wawakilishi mswada wa sheria wa uhakika wa chakula na lishe katika kikao kijacho cha Aprili.

“SMZ imejiandaa kuhakikisha wakulima wananufaika na kukifanya kilimo kuwa kimbilio la vijana wetu… mipango madhubuti imeshawekwa ili kilimo kiwe na tija kwa wakulima wetu na ndio maana Rais wetu, Mheshimiwa Dk. Ali Mohammed Shein mara kwa mara amesisitiza suala la kilimo bora,” alisema Waziri Mansoor.

Waziri huyo alisema uhakika wa chakula na lishe bora ni jambo linalopewa umuhimu wa juu na ndio maana Serikali itawasilisha mswada wa sheria ambapo pia katika sheria hiyo imependekezwa kuwepo kwa ghala la Taifa la akiba ya chakuka Zanzibar.

Alisema kwa sasa hali ya chakula Zanzibar sio nzuri kwani umaskini wa chakula kwa wananchi ni asilimia 13. “hapa kwetu umasikini wa chakula umefikia asilimia 13, Wizara yangu imejikita kuhakikisha tutaondoka katika hali hiyo,” Aliongeza Waziri huyo.

Waziri Mansoor alisema mpango mkakati wa Serikali kwa sasa ni kuwa na uhakika wa chakula na kuongeza kasi ya uzalishaji ili sehemu kubwa ya chakula kizalishwe hapa nchini na kupunguza uagiziaji.

Alisema mabadiliko ya tabia ya nchi yanaiathiri Zanzibar ambapo kikawaida mvua za kupandia zinanyeshe kati ya mwezi Disemba hadi Machi,lakini hadi wakati huu licha ya wakulima kuburuga mashamba yao,hakuna mvua iliyonyesha.

Alisema katika hali kama hiyo, mkakati zaidi unahitajika katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na uhakika wa chakula, hivyo Serikali inaendelea kubuni mbinu mbalimbali kukabiliana na hali hiyo.

Waziri Mansoor alisema Serikali imejipanga kuhakikisha sekta ya kilimo inaendelea kuwa tegemeo la kuinua uchumi na kuimarisha hali za wananchi kuwa bora zaidi, kuishi katika makazi yaliyo bora na kupunguza umaskini.

No comments:

Post a Comment