Tuesday 1 February 2011

MAUAJI YA VICHANGA YALAANIWA.

Mauaji ya vichanga yalaaniwa



Na Mwanajuma Abdi

MKURUGENZI wa Haki za Binadamu, Francis Nzuki, amesema kuzikwa kwa vichanga 10 katika kaburi moja huko Mwananyamala kwa Kopa, ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.

Mkurugenzi huyo alisema hayo jana alipokuwa akifanya mahojiano na gazeti hili, hoteli ya Zanzibar Beach Resort, baada ya kumalizika mafunzo ya wiki moja ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na Tume hiyo.

Mafunzo hayo yaliwashirikisha wadau kutoka Jeshi la Polisi, Mafunzo, KMKM Tanzania Bara na Zanzibar.

Alisema kuzikwa vichanga hivyo katika kaburi moja (kwenye shimo la taka lililokuwa linatumiwa na wananchi, wakiwa wamezongwa shuka lenye lebo ya Bohari Kuu ya Madawa (MSD) ya hospitali ya Mwananyamala, ni kitendo kisichopaswa kunyamaziwa kwani kimekiuka haki za binadamu.

Alieleza tayari wameshaituma timu yao kufuatilia tukio hilo la kinyama, kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa kina ili wahusika waliofanya mambo hayo waweze kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Aidha aliwakemea baadhi ya madaktari wanaojihusisha na utoaji wa mimba, ambao wanachangia kwa kiasi kikubwa kuua viumbe vinavyotarajia kuja duniani.

Alifahamisha kuwa, tukio hilo linaonesha utata mkubwa kwa vile maiti hizo zimefunikwa shuka la hospitali, hivyo alionesha wasiwasi wake kwamba baadhi ya wauguzi wanahusika na mauaji wa watoto hao waliokuwa hawana hatia.

Mkurugenzi huyo, alisema mtoto ana haki tokea anapokuwa tumboni kwa mama tangu wa siku moja hadi anapozaliwa.

Hata hivyo alieleza masuala ya haki za binadamu ni endelevu duniani kote, hivyo ametoa wito kwa jamii kuheshimu uhuru wa mwenzake na kujua haki yake na wajibu wake katika kuhakikisha hakiuki matakwa ya msingi iliyowekwa katika Umoja wa Mataifa juu ya utekelezaji huo.

Nao washiriki mbali mbali walisikitishwa na habari hizo, ambazo walisema kutokana na mafunzo waliyoyapata kuna ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.

No comments:

Post a Comment