Tuesday 1 February 2011

MAFUNZO USHIRIKIANO NI NGUZO UPATIKANAJI HAKI ZA BINAADAMU.

Mafunzo, ushirikiano ni nguzo upatikanaji haki za binadamu

Na Salum Vuai


IMEELEZWA kuwa suala la upatikanaji wa haki za binadamu linahitaj utendaji wa pamoja kati ya taasisi zinazohusika na utoaji haki na jamii ili kuhakikisha kila raia anahudumiwa kwa njia stahiki.

Aidha, mafunzo juu ya mbinu za kufanya upelelezi unaolenga kujua kama haki inatendeka, yameelezewa kuwa muhimu hasa kwa kipindi hichi ambacho dunia inakabiliwa na mabadilko ya sayansi na teknolojia.

Akifunga semina ya siku tisa jana juu ya ufahamu wa uchunguzi na utendaji haki iliyofanyika katika hoteli ya Zanzibar Beach Resort Mazizini, Katibu Mtendaji wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Tanzania Mary Massay, alisema kujifunza ni jambo linalohitaji kuendelezwa.

Alifahamisha kuwa kutokana na umuhimu huo, Tume hiyo itahakikisha inaendelea kuwapatia watendaji wake mafunzo ya mara kwa mara ili kuwapa njia sahihi na zinazokwenda na wakati katika ufanyaji kazi zao.

Alisema kuwa watendaji wa taasisi muhimu zinazotumainiwa kutoa haki kwa umma, ni lazima wajue mbinu mbalimbali za uchunguzi, kuwahoji mashahidi, waathirika wa matendo ya jinai, watuhumiwa, mateso au vifo ndani ya mahabusu na udhalilishaji wa kijinsia sambamba na kuandika ripoti.

Alieleza matumaini yake kuwa washiriki wa semina hiyo wamepata uelewa wa kutosha na kwamba watayatumia mafunzo hayo katika kuwasaidia wanajamii kupata haki, pamoja na kuwa mabalozi kwa wengine ndani ya taasisi zao na katika jamii inayowazunguka.

Aidha alisema kukusanyika kwao hapo, kumesaidia kujenga uhusiano na urafiki ambao kwa njia moja au nyengine utatoa mchango katika dhamira ya kufanikisha kazi za utoaji haki kwa walengwa.

Massay alizishukuru taasisi zote zilizowezesha kufanyika kwa semina hiyo, akizitaja kuwa ni APCOF ya Afrika Kusini, ICD ya Pretoria Afrika Kusini pia, Kituo kinachoshughulikia migogoro na usuluhishi (CSVR) pamoja na taasisi ya GIZ (zamani GTZ).

Mapema akitoa ufafanuzi juu ya lengo la kufanyika mafunzo hayo, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria katika Tume ya Haki za Binadamu Tanzania, Nabor Balthazar Assey, alisema ni kuwapatia mafunzo yanayokwenda na wakati watumishi wake kulingana na mahitaji ya wakati uliopo.

Alieleza kuwa Tume hiyo katika utendaji wake, imegundua mapungufu kadhaa ambayo ni lazima yafanyiwe kazi ili kujenga imani kwa wananchi wanaohitaji haki.

Alizitaja taasisi kubwa ambazo zinategemewa kutoa haki kuwa ni pamoja na Polisi, Magereza, Vyuo vya Mafunzo na Kikosi Maalumu cha Kuzuia Magendo ambazo zote zilitoa washiriki katika semina hiyo.

Mafunzo hayo yalifanyika kwa makundi mawili, moja likianza Januari 24 hadi 28, na jengine Januari 29 hadi jana Februari 1, ambapo washiriki walitoka katika Jeshi la Polisi Tanzania na Zanzibar, Magereza, Vyuo vya Mafunzo na KMKM.

No comments:

Post a Comment