Tuesday, 22 February 2011

MHASIBU WA POLISI KIZIMBANI KWA TUHUMA YA WIZI WA MAMILIONI.

Mhasibu wa Polisi kizimbani tuhuma wizi wa mamilioni

Mwengine jela miaka miwili shambulio la aibu
Na Ali Chwaya Pemba

POLISI Mkoa wa Kaskazini Pemba, imemfikisha Mahakamani Mhasibu wake, Hamad Bakari Faki kwa tuhuma za kuiba fedha za askari wenzake ambazo ni mikato kwa ajili ya Benki ya watu wa Zanzibar.

Akisoma hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Makame Khamis Ali wa Mahakama ya Mkoa Kaskazini Pemba, Muendesha Mashitaka ambaye ni Mwanasheria wa Serikali katika Afisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Ali Haidar Mohammed alidai kuwa kati ya Julai na Disemba 2009, mtuhumiwa Hamad (44) mkaazi wa Bopwe Wete, akiwa mtumishi wa Serikali aliiba shilingi 33, 428,670 /70

Alisema kitendo hicho ni kosa chini ya sheria na kudaiwa alifanya kitendo hicho katika mikato mbali mbali ya malipo ya askari kupitia Benki ya watu wa Zanzibar PBZ.

Mtuhumiwa Hamad alikana madai hayo na yuko nje kwa dhamana hadi Machi 21, 2011 kesi yake itakapotajwa tena.

Katika masharti ya dhamana, alitakiwa kuweka dhamana ya Tshs milioni 40 za maandishi na wadhamini wawili kwa shilingi milioni 10 kila mmoja za maandishi na mmoja wao awe mtumishi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Wakati huo huo, Rashid Hamad Faki (18)mkaazi wa Kizimbani Wete, ambaye alikuwa akikabiliwa na mashitaka matatu katika mahakama hiyo ikiwemo Shitaka la ubakaji, utoroshaji na shambulio la aibu, mahakama ya Mkoa Wete, imemfutia shitaka la ubakaji na utoroshaji baada ya upande wa mashtaka kushindwa kumuunganisha katika ushahidi uliotolewa.

Awali ilidaiwa mahakamani hapo na Mwendesha Mashitaka kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, Ali Haidar Mohamed kuwa Oktoba 10, 2009, usiku, huko Mtemani Wete, Mtuhumiwa huyo alimtorosha, kumbaka na kufanyia shambulio la aibu msichana huyo (16) aliekuwa chini ya uangalizi wa wazazi wake.

Hata hivyo mahakama ilimtia hatiani, Rashid Hamad Faki (18), kwa kosa moja la Shambulio la aibu na kumuamuru kwenda Chuo cha Mafunzo miaka miwili licha ya Mwendesha Mashitaka kuomba kutolewa adhabu kali kwa mujibu wa Sheria.

No comments:

Post a Comment