Wednesday, 23 February 2011

FAMILIA 10 MIKUNGUNI ZAKUMBWA NA MARADHI YA KUHARISHA.

Familia 10 Mikunguni zakumbwa na maradhi ya kuharisha


Na Mwandishi wetu

WATU kutoka zaidi ya familia 10 katika Shehia ya Mikunguni, wamekumbwa na maradhi ya kuharisha baada ya kutumia maji yasiyo salama yanayosadikiwa kuchanganyika na kinyesi cha binadamu.

Tatizo hilo limewakumba zaidi watoto baada ya kutumia maji hayo yaliyokuwa na ladha ya uchungu pamoja na rangi ya udongo.

Katika taarifa yake kwa Zanzibar Leo, Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA), imesema hali hiyo imesababishwa na mwananchi mmoja katika eneo hilo kujenga shimo la karo na kusababisha kinyesi kuchanganyika na maji safi baada ya bomba la maji la chini ya ardhi kupasuka kwa kemikali za kinyesi.

Afisa Uhusiano wa ZAWA, Zahor Suleiman alisema katika kukabiliana na tatizo hilo, Mamlaka lichukua hatua ya kufunga laini ya maji katika eneo hilo na kubadilisha mfumo mzima wa usambazaji maji ili yasipite kwenye karo hilo.

Mabadiliko hayo, yamesababisha wananchi wa shehia hiyo kukosa huduma za maji na kusababisha usumbufu mkubwa, hata hivyo hatua hiyo imechukuliwa ili kunusuru maisha ya wananchi na kuhakikisha wanapata huduma ya maji safi na salama kwa wote.

Shehia ya Mikunguni kwa muda mrefu imekuwa ikikosa huduma za maji safi kutokana na uchakavu wa miundombinu, lakini wakati ZAWA ikiweka laini mpya baada ya siku tatu tu hali ya maji ilibadilika na kuwa na ladha ya uchungu.

No comments:

Post a Comment