Thursday, 26 August 2010

TUKIO LA UVUNJWAJI MEZA MWANAKWEREKWE


Waliovunja ni wahuni - Halmashauri


L Manispaa kuburuzwa mahakamani


Husna Hamid na Hamisuu Abdalla, MCC
KADHIA ya uvunjwaji wa meza za wafanyabiashara katika soko la Mwanakwerekwe imeingia katika sura mpya, baada ya Halamshauri ya Wilaya ya Magharibi kueleza uvunjwaji huo umefanywa na wahuni.

Afisa mmoja katika Halmshauri hiyo, alilieleza gazeti hili kuwa hawaamini kama Baraza hilo linaweza kuchukua uamuzi wa kuzivunja meza za wafanyabishara hao, ikizingatiwa kuwahi kufanyika mazungumzo baina ya Halmashauri hiyo, Baraza la Manispaa pamoja na Waziri Kiongozi wa Zanzibar, Shamsi Vuai Nahodha.

Afisa huyo ambaye alikataa katakata kutajwa jina lake gazetini, alisema kutokana na mazungumzo yaliyozishirikisha pande hizo, Manispaa haiwezi kuzivunja meza za wafanyabiashara hao ambao walitengewa eneo hilo kwa ajili ya kuondosha msongamano ndani ya soko kuu la Mwanakwerekwe.

"Manispaa haiwezi kuzivunja meza hizo kwani wanafahamu vilivyo uwepo wa wafanyabiashara nyuma ya soko hilo kufuatia mazungumzo ya pamoja tuliyowahi kuyafanya, nadhani waliovunja meza za wafanyabishara ni wahuni",alisema Afisa huyo.

Afisa huyo alithibitisha kuwa Halmashauri iliwapa wafanyabiashara eneo hilo kwani liko chini ya milki yao kwa mujibu wa sheria nambari 4 ya mwaka 1995.

"Hata hili soko liko kwenye eneo letu kwa mujibu wa mamlaka ya kiutawala lakini serikali imeamua kuwapa Manispaa", alisema.

Wakati huo, Afisa Habari wa Baraza la Manispaa alishindwa kutoa ushirikiano wa kutosha kwa waandishi wa habari ambapo waliwataka waende kwa Mkuu wa Mkoa kutafuta habari hizi.

Naye Mohammed Gharib wa ZJMMC, anaripoti kuwa wafanyabiashara waliovunjiwa meza wanakusudia kuliburuza mahakamani Baraza la Manispaa la Zanzibar ambalo wanalituhumu kuhusika na uvunjaji wa meza hizo.

Katibu wa kamati ya wafanyabiashara hao Mkubwa Khamis Hamad alisema wameshafungua kesi katika kituo cha Polisi Mwanakwerekwe na wanachosubiri taratibu za sheria zitakazochukuliwa na jeshi hilo.

Mkubwa alisema katika jalada walilofungua kituoni hapo, malalamiko yao ya msingi ni kuvunjiwa meza zao mpya 13 ambapo kila moja meza ina gharama ya shilingi 130,000.

Alisema mbali ya meza hizo pia baraza hilo limevunja meza ndogo ndogo zipatazo 70 ambapo wamechukua hatua hiyo kinyume na utaratibu.

Katibu huyo alifahamisha kuwa pia eneo hilo ambalo meza zao zimevunjwa waliliwekea kifusi gari nane huku kila gari moja ikigharimu shilingi 130,00.

"Waliingia na kuvunja kupitia lango kubwa la soko na baada ya kufika hapa walimuamuru mlinzi wetu aondoke na kuzivunja meza zetu", alisema Katibu hiyo.


Nao Salma Lusangi (ZJMMC), Kassim Kassim (TUDARCO), wanaripoti kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mjini na Magharibi Abdalla Mwinyi Khamis ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Magharibi na Baraza la Manispaa kuzungumza kuutafutia ufumbuzi mgogoro huo.

Alisema alimuomba Mkurugenzi wa Manispaa awaachilie wafanyabiashara hao kuendelea na biashara zao katika eneo hilo kwa kipindi hichi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani huku likitafutiwa ufumbuzi wa kudumu suali hilo juu ya nani mmiliki halali wa eneo hilo.

Aidha Katibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Magharibi alithibitisha juu ya kuwaruhusu wafanyabiashara hao kuwepo katika eneo hilo huku wakijua ni sehemu ya Halmashauri kutokana na sheria nambari 4 ya mwaka 1995.

Alisema siku nyingi eneo hilo lilikuwa na mgogoro baina yao na Baraza la Manispaa wakidai ni eneo lao lakini Wizara husika itaendelea kushughulikia suali hilo.

Aidha alisikitika kwa kitendo walichofanyiwa wafanyabiashara hao bila kuarifiwa juu ya uamuzi wa kuondolewa eneo hilo wakati serikali inahimiza vijana kujiajiri wenyewe katika kujitafutia riziki zao za halali.

No comments:

Post a Comment