Thursday 26 August 2010

MICHEWENI BADO WALIA NA AJIRA ZA WATOTO

Micheweni bado walia na ajira za watoto

Zaidi ya 100 hukosa kuhudhuria masomo kwa mwezi

Na Bakari Mussa, Pemba

ZAIDI ya watoto 100 katika Skuli ya Msingi Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba wanakosa fursa ya kuhudhuria skuli kila mwezi.

Mwalimu Mkuu skuli ya msingi, Micheweni Kai Pandu Kai amesema idadi hiyo ni kati ya wanafunzi 1,720 wa Skuli, ambao wamebainika kujihusisha na ajira za watoto.

Alisema umasikini wa kipato umesababisha ongezeko ajira zisizokuwa salama kwa watoto, hali ambayo imeathiri zaidi vijiji vya Micheweni na Vitongoji vyake.

"Watoto wanne hadi watano wanakosa masomo kila siku kwa kila darasa na kubakia wastani wanafunzi 58 kila darasa.

Aliendelea kusema kuwa Skuli imekuwa ikishirikiana na kamati mbali mbali za Vijiji na Shehia wakiwemo Wazazi lakini imeonekana baadhi ya Wazazi kuwa na mawazo finyu juu ya suala hilo kwa kisingizio cha Umaskini wa kipato.

Unapomwambia mzazi juu ya kumpeleka mtoto wake skuli anakwambia yeye hana uwezo labda umsaidie….. wakati na wewe una wako anataka elimu,” alisema mwalimu huyo.

Aliongeza kuwa tatizo la ajira za watoto lipo katika Skuli ya Micheweni na lina athari kubwa kwa vile wanafunzi walio wengi huwa hawaendi skuli kikawaida.

Hata hivyo, alisema skuli yake imeanza kupata unafuu kutokana na misaada inayopata kupitia kamati mbali mbali za taasisi zisizokuwa za kiserikali kama PIRO, yenye Makao makuu Chake Chake, Pemba.

Kwa jumla Mwalimu huyo alisema baada ya wazazi kupatiwa taaluma ya kutosha sasa wameamua kuwarejesha watoto wao skuli badala ya utaratibu wa zamani ambapo walikuwa wakiwapeleka malezini na kuingia kwenye ajira mbaya.

Msaidizi Mwalimu Mkuu wa Skuli hiyo, Omar Mwinyi Suwed, alisema skuli hiyo imepoteza wanafunzi watatu waliofariki mwaka 2008/2009 kwa kujihusisha na ajira za uchimbaji mawe baada ya muda wa skuli na wengine wawili walipoteza maisha kwenye uchimbaji mawe.

Aidha, Msaidizi Mwalimu huyo alisema pamoja na hali ya umasikini lakini ushirikiano mdogo kati ya walimu na uongozi wa majimbo huchangia kuwepo ajira hizo.

Ajira zinazowavutia vijana hao ni pamoja na uvunjaji wa mawe, kupara Samaki, uchungaji wa mifugo, uvuvi na ukataji wa matufali na wanaojihusisha zaidi ni wanafunzi wa msingi kuanzia darasa la kwanza hadi la Saba.

Katika hali kama hiyo, Mwalimu Muu wa Sekondari Micheweni, Mutrib Hamad Mbarouk , alisema wanafunzi 80 hadi 100 wa Sekondari Micheweni Pemba, hawahudhurii skuli kila siku, wengi wao wakiwa katika ajira hizo.

Mwalimu mkuu huyo wa Sekondari ya Micheweni Pemba aliwahimiza wazee kufahamu faida ya elimu na kusema rasilimali pekee inayomfaa mtoto ni elimu na sio ajira ya Muda.

Alisema bila elimu maisha ya binadamu yanakosa baadhi ya mambo hivyo akahimiza watoto wsapatiwe elimu ili hatimae wajiendeshee maisha yao kwa uhakika zaidi.

Pamoja kuzungumzia wanafunzi wa madarasa ya chini lakini mwalimu huyo alisema hata wanafunzi wa elimu ya juu nao wanavutika na ajira hizo na kuathiri mwenendo wao wa masomo.

“Tunashirikiana na Kamati ya Skuli na Walimu wa Ushauri Nasaha, Masheha na Watu maarufu wa Vijiji kupita kwa Wazazi kuwaeleza tatizo la watotowao na ajira hizo ingawaje mafanikio sio makubwa” alisema.

Hata hivyo, afisa elimu Mkoa wa Kaskazini Pemba, Hassan Sheha, amesema kwa upande wa Afisi yake hajapokea kesi ya aina yoyote juu ya sula hilo hata mara moja na yeye anasikia hivo hivo.

"Zamani sana alipokuwepo Kamanda wa Polisi Mbirikira, katika Mkoa wa Kaskazini, yeye alikuwa ananieleza pindipo akipata kesi za aina hiyo,” alimaliza afisa huyo.

Micheweni ni eneo ambalo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imwekeza nguvu nyingi na kukifanya ‘Kijiji cha Milenia’, ili kuhakikisha inawakomboa wananchi wa eneo hilo na umasikini.

Aidha huduma mbali mbali muhimu za kijamii kama vile barabara, afya na elimu, zimeimarishwa kimiundombinu, ikiwa ni kijiji cha mfano wa kupambana na umasikini Zanzibar, lakini bado muamko na kubadilika wananchi wake ni kudogo.

No comments:

Post a Comment