Wednesday 25 August 2010

WALIMU WALIOSIMAMISHWA CHUO CHA KIISLAM UTETEZI WAO KUZINGATIWA LEO.

Walimu waliosimamishwa Chuo cha Kiislamu utetezi wao kuzingatiwa leo


Na Mwantanga Ame (ZJMMC)

BAADA ya Uamuzi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar kuusimamisha Uongozi wa walimu wa Chuo cha Kiislamu Zanzibar, leo Wizara hiyo inakusudia kukaa na kulizungumzia suala hilo.

Uongozi huo ulisimamishwa wiki mbili zilizopita akiwemo Mkuuwa chuo, baada ya Wizara hiyo kubaini kuwapo kwa baadhi ya walimu kuhusishwa na mchezo mchafu wa kupokea rushwa kutoka kwa wanafunzi .

Uamuzi wa kusimamishwa walimu hao ulitokana na madai ya kuwepo wanafunzi ambao waliingia katika Chuo hicho kwa njia ambazo hazikustahili kwa vile walikosa sifa za kujiunga na chuo hicho kwa ngazi ya Stashahada.

Kubainika hilo Wizara hiyo iliamua kuwasimamisha baadhi ya wanafunzi waliobainika kufanya udanganyifu huo ambao walikuwa wakiendelea kuchuku mafunzo kwa ngazi ya Stashahada.

Mbali ya kusimamishwa kwa wanafunzi hao Wizara hiyo pia iliwataka walimu wa hao kuwarejeshea fedha walizozitoa wanafunzi hao kwa ajili ya kujiunga na Chuo hicho.



Akizungumza na Zanzibar Leo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Abdllah Suleiman alisema uongozi wa Wizara hiyo unakusudia kulifanyia kazi suala hilo leo ambapo kutakuwa na kikao cha kutathmini tukio hilo.



Alisema hatua hiyo Wizara inaichukua baada ya kuwapa muda walimu wanaodaiwa kuhusika na tukio hilo kutoa maelezo yao juu ya kujitetea.



Alisema katika kikao hicho Wizara hiyo itapitia utetezi huo na baadae kuona ni hatua zipi itaweza kuzichukua kwa vile walimu hao hivi sasa wamesimamishwa ili kuweza kupisha uchunguzi kufanyika juu ya tukio hilo.



Naibu huyo alieleza kuwa kikao kitachokaa leo kitakuwa ni cha ndani ambapo kitauhusisha uongozi wa juu pekee wa Wizara hiyo baada ya wadaiwa hao kumaliza kutoa utetezi wao.



Hata hivyo, hakueleza wazi kama kikao hicho baada ya kumaliza kama kitakuwa ndio hatma ya tukio hilo kwani kitazingatia na upande mwengine kama utahitaji kufanyiwa kazi zaidi.

No comments:

Post a Comment