Thursday 19 August 2010

MAREKEBISHO YA 10 YA KATIBA YA ZANZIBAR

MAREKEBISHO YA 10 YA KATIBA YA ZANZIBAR



Hakuna uvunjaji Katiba ya Jamhuri - Wanasheria


 Wasema yameondoa utata kuhusu tafsiri na hadhi ya Zanzibar


Wanahabari, Wanasheria wasichochee kuharibu muungano


Na Mwandishi wetu

MAREKEBISHO ya 10 ya katiba ya Zanzibar yaliyofanywa na kikao cha Baraza la Wawakilishi kilichomalizika hivi karibuni hayakwenda kinyume wala kuvunja katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wakizungumza na gazeti hili wanasheria mbali mbali waandamizi walisema hakuna kipengele cha katiba ya Jamhuri ya Muungano kilichoivunja kufuatia marekebisho hayo.

Walisema kufutwa kwa kifungu cha pili cha Katiba ya Zanzibar kilichorekebishwa na kuandikwa upya kinachosomeka kuwa Zanzibar ni miongoni mwa nchi mbili mbili zinazounda Jamhuri ya Muungano ni jambo lililo wazi na ndivyo uhalisia lilivyo kama ilivyoelezwa katika Katiba hiyo ya Jamhuri ya muungano inayodaiwa kuvunjwa.

Wanasheria hao walisema Tanzania imeundwa na nchi mbili zilizo huru ambazo ni iliyokuwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya watu wa Tanganyika, na hivyo kilichopotea ni utaifa wa Jamhuri hizo zilizoungana na si nchi.

"Kutokana kuwepo kwa Muungano huu Zanzibar na Tanganyika zimepoteza Utaifa na kubakia Utanzania lakini nchi ya Zanzibar bado ipo ndani ya Tanzania na hata kama Tanganyika wanataka iwepo hilo ni juu yao", alisema mmoja kati ya Wanasheria hao.

Walisema suala hilo sio geni kwani Marekani inaundwa na nchi 52 huku kila nchi ikiwa na sheria zake, mambo mengine ya kiutawala na kiuendeshaji lakini wanaunganishwa na taifa moja la Marekani.

"Kama mabadiliko ya katiba ya Zanzibar yaliyofanywa yangeielezea hiyo Nchi ya Zanzibar nje ya mipaka ya Tanzania hilo tungeliita uvunjwaji wa Katiba ya Jamhuri vyenginevyo Katiba haijavunjwa", alieleza.

Wakielezea kifungu 26(1) cha katiba ya Zanzibar kilichofutwa na kuandikwa upya kama kinavyosomeka kutakuwa na Rais wa Zanzibar ambaye atakuwa mkuu wa Nchi ya Zanzibar, Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, walisema kipengele hicho kimelenga kuainisha, kufafanua na kuweka wazi Nchi itakayoongozwa na Rais huyo, ili isilete tafsiri yenye utata kama ilivyo mambo mengi yanayohusiana na muungano hivi sasa.

Walisema Zanzibar ina haki na Mamlaka yake Kikatiba ambayo inaweza kuyafanyia maamuzi bila kuhitaji kupitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ikiwemo kutangaza mipaka yake na kufanya hivyo sio kosa ilimradi mipaka hiyo imo ndani ya Taifa la Tanzania.

Kauli hiyo kwamba Zanzibar ina uwezo wa kutangaza mipaka yake ndani ya Tanzania, imeelezwa pia na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alipozungumza na waandishi wa habari kuhusiana na mabadiliko hayo ya 10 ya Katiba ya Zanzibar.

Naibu Mwanasheria huyo wa Serikali ya Tanzania, aliwataka waandishi wa habari waache kuchochea migogoro kwa kuibua mambo ambayo si sahihi na hayana msingi, bali walenge zaidi kuripoti mambo yatayoimarisha umoja nchini.

Aidha wanasheria hao wamesema Zanzibar si Nchi moja, bali ni Taifa moja kwa kueleza kuwa hata Nchi ya Tanganyika bado ipo kupitia Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wakizungumzia juu ya kufutwa na kuandikwa upya kifungu kinachompa Mamlaka Rais wa Zanzibar kugawa mikoa na wilaya bila ya ushauri wa Rais wa Jamhuri, walisema suala la Tawala za Mikoa halimo katika orodha ya mambo ya Muungano, hivyo hakuna kosa Katiba ya Zanzibar kuainisha hilo.

"Tawala za mikoa si suala la Muungano, Rais wa Zanzibar ana haki ya kuigawa Zanzibar kijiografia katika kuwaharakishia maendeleo wananchi wake vyovyote apendavyo, bila ya kushauriana na Rais wa Jamhuri kwani suala la Serikali za Mitaa si suala la Muungano au wanaolalamika watueleze vyenginevyo".

Walisema marekebisho hayo yametafsiri kwa uwazi hadhi ya Zanzibar katika muungano na kuondosha utata wa tafsiri ambao umekuwa ukitokea mara kwa mara, jambo ambalo litasaidia kuimarisha muungano huo.

Vyombo vya habari na baadhi ya wanasheria wakiyalalamikia marekebisho hayo yaliyopitishwa hivi karibuni na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar kwa kudai, Katiba ya Jamhuri imekiukwa na Baraza la Wawakilishi kwa kufanya marekebisho hayo.

Mwanasheria maarufu nchini Tanzania, Profesa Issa Shivji, hivi karibuni kupitia kipindi cha televisheni cha 'Hamza Kasongo Hour', alitoa ufafanuzi wa suala hilo na kusema kuwa hakuna uvunjaji wa katiba uliofanyika katika marekebisho hayo.

Wanasheria wengine wamekwenda mbele zaidi na kueleza kwamba, hata 'sovereignity' ya Tanzania nayo kiutendaji imegawika, ambapo sehemu yake imebakia Zanzibar, katika mambo yanayoitwa si ya Muungano na sehemu nyengine imechukuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mambo yaliyo ya muungano na yale yasiyo ya muungano kwa upande wa Tanzania Bara.

No comments:

Post a Comment