Tuesday, 17 August 2010

MAMA SHADYA AHUTUBIA WAKE WA VIONGOZI WA SADC.

MAMA SHADYA AHUTUBIA WAKE WA VIONGOZI WA SADC NA KUSEMA


Wanawake wa Zanzibar wamepiga hatua kubwa kimaendeleo

Wanashiriki katika nyanja zote ikiwemo siasa, uchumi

Watoto wa kike wanapata fursa sawa na wa kiume

Aeleza mafanikio sekta ya afya ya mama na mtoto

Rais Karume na ujumbe wake kurejea leo

Na Rajab Mkasaba, Namibia

MKE wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mama Shadya Karume, amesema hatua kubwa imefikiwa Tanzania hasa Zanzibar katika kuhakikisha wanawake wanapata mafanikio katika maendeleo ya kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiutamaduni.

Mama Shadya Karume aliyasema hayo katika mkutano maalum wa wake wa viongozi wakuu wa Jumuiya ya SADC waliohudhuria katika mkutano wa siku mbili wa SADC, unaofanyika katika mji mkuu wa Namibia, Windhoek.

Katika maelezo yake Mama Shadya Karume alisema kuwa kwa upande wa Zanzibar hatua kubwa zimefikiwa ambapo wanawake wamepata fursa ya kushiriki kikamilifu katika nyanja zote za kimaendeleo.

Akitoa mfano katika sekta ya elimu Zanzibar, Mama Shadya Karume alieleza kuwa watoto wa kike wamekuwa wakipata fursa sawa na wanaume katika sekta hiyo muhimu na tayari mafanikio makubwa yamefikiwa kwa upande wa wanawake kwenye sekta hiyo ya elimu. “Tayari asilimia mia moja ya watoto wa kike Zanzibar wamepata fursa ya kujiunga na skuli”, alisema Mama Shadya Karume.

Mama Shadya Karume alisema kuimarika kwa sekta ya afya kumewawezesha akinamama na watoto kupata huduma hiyo kwa urahisi kwani tayari kwa kila pembe ya Zanzibar yenye eneo la  kilomita tano pana kituo cha afya.

Aidha, Mama Shadya Karume alisema kuwa kwa kutambua umuhimu wa wanawake katika jamii Serikali ya Mapinduzi Zanzibar miongoni mwa Wizara zake ipo Wizara maalum inayoshughulikia Wanawake na Watoto, ambayo ni Wizara ya Kazi, Maendeleo ya Vijana, Wawanawake na Watoto inayoongozwa na Waziri mwanamke.

Alieleza kuwa mifuko mbali mbali ya kuwawezesha wanwake kimaendeleo imeimarishwa ili kuwa saidia wanawake katika kujikwamua kiuchumi ukiwemo mfuko wa (WEDTF).

Mama Shadya alieleza kuwa kuna umuhimu mkubwa wa kuimarisha sekta ya afya ili wanawake wazidi kupata huduma muhimu.

Katika hotuba yake alitoa wito kwa wake wa viongozi wa nchi wanachama wa SADC kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazowakabili wanawake barani Afrika.

Sambamba na hayo, Mama Shadya Karume alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar  imeweza kutoa ushirikiano na misaada yake kwa Jumuiya zisizo za kiserikali (NGOs) ambazo husaidia wanawake.

Mama Shadya Karume alisema kuwa katika kuhakikisha wanawake wanapata maendeleo kisiasa, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Baraza lake la Wawakilishi, Wajumbe wanawake wameweza kufikia asilimia 30 kwa sasa ambapo lengo ni kufikia asilimia 50.

Pamoja na hayo, Mama Shadya Karume alieleza kuwa licha ya mafanikio yaliopatikana lakini bado kuna changamoto ambazo tayari Serikali inazifanyia kazi ili kuweza kupata mafanikio na maendeleo zaidi kwa wanawake.

Mama Shadya Karume alitoa pongezi  na shukurani kwa Mke wa Rais wa Namibia Mama Penehupifo Pohamba kwa ukarimu na mafanikio yaliopatikana nchini kwake pamoja na mafanikio ya Mkutano wa SADC ambapo Jumuiya hiyo imetimiza miaka 30 tokea kuundwa kwake.

Miongoni mwa wake wa viongozi wa SADC waliohudhuria katika mkutano huo ni  Mke wa Mfalme wa Swaziland, Malkia Lambikiza, Mke wa Rais wa Zambia Mama Thandiwe Banda, Mama Matho Mosisili, Mke wa Rais wa Lesotho, Mke wa Rais wa Namibia Mama Penehupifo Pohamba.

Mkuu wa Mkoa wa Khomas ambao ndio Mkoa mwenyeji wa shughuli hizo za SADC, Mama Sophia Shaningwa alimpongeza Mama Penehupifo Pohamba kwa kuweza kuwaunganisha wake wa viongozi kwa kuweza kukaa pamoja kwa lengo la kueleza masuala mbali mbali ya wanawake katika mkutano huo.

Katika hotuba yake hiyo, Mama Shaningwa alisisitiza haja ya wake wa viongozi hao wakuu wa SADC kuwaeleza viongozi wakuu umuhimu wa kuwashajihisha na kuimarisha matumizi ya bidhaa za soko la ndani ili kuwapa manufaa wanawake.

Wakati huo huo, Mama Shadya Karume aliungana na wake wa viongozi wakuu wa nchi Jumuiya ya SADC katika kuhudhuria maonyesho ya kazi za mikono za akinamama wa nchi wanachama wa SADC ikiwemo Tanzania, yaliyofanyika mjini Windhoek.

Mama Shadya Karume amefuatana na mumewe Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Amani Abeid Karume kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali za Jumuia ya Ushirikiano Kusini mwa Afrika (SADC), akimuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete.

Rais Karume na ujumbe wake wanatarajiwa kurejea nchini leo mchana.

No comments:

Post a Comment