Friday, 27 August 2010

Rais Karume Ashuhudia Kenya Ikizaliwa Upya.

Rais Karume ashuhudia Kenya ikizaliwa upya

 Kibaki aeleza matumaini ya mshikamano, maendeleo zaidi
 Wakenya wafurika Uhuru Park kukaribisha Katiba mpya


Na Mwandishi Maalum
WANANCHI wa Kenya jana waliingia katika ukurasa mpya wa historia ya nchi hiyo, baada ya Katiba mpya ya Taifa hilo kuzinduliwa na Rais Mwai Kibaki, katika sherehe kubwa iliyofanyika viwanja vya Uhuru Mjini Nairobi.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Amani Abeid Karume, aliongoza Ujumbe wa Tanzania kushuhudia sherehe hizo kubwa za kuzaliwa upya kwa Jamhuri ya watu wa Kenya.

Dk. Karume aliongozana na viongozi mbali mbali akiwemo Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Benjamin Mkapa, waziri wa Nchi Afisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, anaeshughulikia fedha na Uchumi, Dk. Mwinyihaji Makame na Naibu waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Seif Ali Iddi.

Wengine ni Mwenyekiti wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, Ali Mzee Ali, ambae pia alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Watu Sita ya Baraza la Wawakilishi ya Kusimamia kura ya maoni, pamoja na Makamo Mwenyekiti wake na Mkuu wa Kambi ya upinzani katika Baraza la Wawakilishi, Abubakar Khamis Bakary.

Akihutubia maelfu ya wananchi wa Kenya waliohudhuria sherehe hizo, baada ya kutia saini Mswada huo kuwa Sheria, Rais Mwai Kibaki wa Kenya, alisema Katiba mpya inafufua matarajio ya wananchi wa Nchi hiyo kuhusu mustakbali wa maendeleo yao.

Kibaki aliieleza hadhara hiyo kwamba Katiba hiyo mpya, mbali ya kufungua ukurasa mpya wa historia ya Kenya, pia italibadilisha Taifa hilo kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Akizungumzia changamoto zitazotokana na Katiba hiyo mpya, Rais Kibaki aliwataka wananchi wa Kenya, kujenga matumaini zaidi kwa kuwepo muundo mpya wa uendeshaji nchi hiyo.

Aidha Kibaki aliwataka Wakenya kuitumia Katiba mpya kwa kubadilisha mitazamo na uendeshaji wa masuala ya kisiasa nchini humo.

"Kwa Katiba hii mpya tutabadilisha mitazamo ya kuendesha siasa nchini mwetu, jambo ambalo linategemea kuungwa mkono na Wakenya wote, ili kona zote za nchi yetu ziendelee." alisema Kibaki.

Katika hafla hiyo Rais Kibaki, alikula kiapo cha kuiongoza nchi hiyo kwa kutumia Katiba mpya, ambapo baadae Majaji na Wabunge pia waliapishwa kwa kutumia Katiba mpya.

Akimkaribisha Rais Kibaki kutoka hotuba yake, Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Odinga, alisema kuzinduliwa kwa Katiba hiyo ya Kenya, ambako kumeashiria kuzaliwa kwa mara ya pili Jamhuri hiyo ni kukamilika kwa safari moja na mwanzo wa safari nyengine kwa nchi hiyo.

"Kenya imeamka...hatutaki kurudi nyuma. Utawala mpya umeanza. Uongozi wa Kiimla na dhuluma tumeweka katika kaburi la sahau..." alisisitiza Raila.

Hotuba za sherehe hiyo zilianza kwa Makamo wa Rais wa Kenya, Kalonzo Musyoka kuwapongeza Wakenya kwa uzinduzi wa Katiba mpya.

Msanii maarufu wa Kenya, Eric Wainaina, alitumbuiza hadhara hiyo kwa wimbo maarufu wa 'Daima Kenya', wimbo ambao unapendwa kama wimbo wa taifa na wananchi wa nchi hiyo, kutokana na kutoa wito kwa Wakenya kuwa Wazalendo zaidi.

Pamoja na Rais Karume aliyeiwakilisha Tanzania, wageni wengine maarufu waliohudhuria sherehe hizo ni Katibu Mkuu Mstaafu wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, Mke wa Rais Kibaki, Mama Lucy Kibaki, na Rais Mstaafu wa Kenya, Daniel Arap Moi.

Wengine ni Rais wa Sudan, Omar Hassan Al-Bashir, Rais Abdalla Sambi 'Ayatollah' wa Visiwa vya Comoro, Rais Museveni wa Uganda na Rais Paul Kagame wa Rwanda.

Pia Rais Mstaafu wa Ghana, John Kuffour, Rais Mstaafu wa Nigeria, Olesegun Obasanjo na Mke wa Rais Mstaafu wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, Mama Grace Machel na Mwenyekiti wa Kamisheni Umoja wa Afrika (AU), Jean Ping.

Wananchi wa Kenya waliipitisha Katiba mpya kufuatia kupiga kura za maoni Agosti nne mwaka huu, ili kuunda Kenya mpya baada ya nchi hiyo kukumbwa na ghasia za kisiasa.

No comments:

Post a Comment