Tuesday 24 August 2010

NRA NAYO YASIMAMISHA MGOMBEA URAIS ZANZIBAR

NRA nayo yasimamisha mgombea Urais Z'bar


Mwanajuma Abdi na Kassim Kassim, TUDARCO

MGOMBEA wa Chama cha Muamko wa Umma (NRA), Haji Khamis Haji, jana alijitokeza kuchukua fomu ya kuwania nafasi ya Urais wa Zanzibar katika Makao Makuu ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Maisara mjini hapa.

Mgombea huo amefanya idadi ya wagombea waliochukua fomu za kuwania nafasi ya Urais wa Zanzibar katika Tume hiyo kufikia wanane hadi sasa, ambapo Mkurugenzi wa ZEC, Salum Kassim Ali alimkabidhi fomu mgombea huyo majira ya saa nne asubuhi.

Mkurugenzi huyo wa Tume ya Uchaguzi akimsomea maelezo ya fomu hizo, alimueleza mgombea anatakiwa kuzijaza fomu hizo kwa usahihi, ambapo siku ya mwisho ya kurejesha fomu Agosti 30, majira ya saa 10:00 jioni.

Aidha alimpongeza mgombea huyo kwa uamuzi wake wa kufika afisini hapo kuchukua fomu za kuwania kiti cha Urais Zanzibar.

"Kwa mujibu wa barua ya chama cha NRA ya Agosti 23 kimemteua Haji Khamis Haji kuwa mgombea wake wa kiti cha Urais Zanzibar," alisema Salum.

Nae Mgombea wa Urais kwa tiketi ya NRA, Haji Khamis Haji alisema ameamua kuchukua fomu ili chama chake kiwe mbadala katika kuelekea Serikali ya Umoja wa Kitaifa badala ya kuviacha vyama viwili vyenye ushindani vya muda mrefu vya CCM na CUF.

Alisema chama hicho kimeamua kuingia katika mchakato huo ili kuweza kuleta mageuzi ya kisiasa na kiuchumi nchini.

Wakati huo huo, wagombea wa Udiwani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Yussuf Idrissa anayewania udiwani Wadi ya Magomeni na Takidir Hamad Suleiman anayewania Wadi ya Meya wamerejesha fomu za uteuzi wa nafasi hizo katika Afisi ya Tume ya Uchaguzi Wilaya ya Mjini Unguja jana.

Msimamizi wa Uchaguzi Wilaya ya Mjini, Mwanapili Khamis Mohammed alizipokea fomu hizo baada ya kuzifanyia uhakiki na kuwataka wagombea hao kufika katika Afisi hiyo Agosti pili, majira ya saa 10:00 jioni, kuja kuangalia pingamizi ama wao kama wanataka kuwawekea pingamizi wagombea wenzao.

Wagombea hao wamefika majira saa tano asubuhi katika Afisi hiyo wakiwa wameongozana na mapikipiki na gari mbali mbali.

No comments:

Post a Comment