Saturday 21 August 2010

VIKOSI VYAPIGWA MSASA MAANDALIZI UCHAGUZI MKUU.

Vikosi vyapigwa msasa maandalizi uchaguzi mkuu

Na Zainab Mtima, ZJMMC

JESHI la Polisi Makao Makuu Dar es salaam, limekuwa likiwapatia mafunzo ya kuvijengea uwezo vikosi vya ulinzi na usalama ili viweze kufanya kazi zake kwa ufanisi zaidi wakati wa uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba 2010.

Akizungumza katika mafunzo hayo mkufunzi kutoka Dawati la Uchaguzi la Jeshi la Polisi Makao Makuu, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Nasser Edward alisema lengo ni kuvijengea uwezo vikosi vinavyoshiriki katika uchaguzi.

Mkufunzi huyo alisema lengo la mafunzo hayo ni kuufanya uchaguzi mkuu kuwa huru na wa haki kwa wananchi na wapiga kura kwa ujumla.

Alisema mafunzo hayo ni ya kwanza kuwahi kufanywa hapa zanzibar na kuvishirikisha vikosi vyote vya ulinzi na usalama.

Mrakibu huyo alisema muda umefika kwa vikosi vinavyo simamia uchaguzi kujua haki za raia na walivyo na wajibu wa kuvilinda na kuvisimamia kwa vitendo haki za wananchi na wapiga kura.

Hata hivyo mshiriki wa mafunzo hayo kutoka Jeshi la Kujenga Uchumi, JKU, Kapteni Waziri Khamis, amesema mafunzo hayo yatawasaidia kusimamia masuala ya uchaguzi na kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na wa haki.

Mafunzo hayo ya wiki mbili yanayofanyika Chuo cha Polisi Ziwani, yanawahusisha Polisi, JWTZ, JKU,KMKM, Valantia, Chuo cha Mafunzo na kikosi cha Zima moto na Uokozi.

Mafunzo hayo yanaandaliwa na Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kupitia mradi wa kusaidia uchaguzi (ESP)

No comments:

Post a Comment