Monday 30 August 2010

2,000,000/ ZASABABISHA MMOJA ANG' OKE MBIO ZA URAIS ZANZIBAR.

2,000,000/ zasababisha mmoja ang'oke mbio za Urais Z'bar


 Akimbilia Mkwajuni kujaza fomu za Uwakilishi


 Wagombea wanne wafanikiwa kuzirejesha jana

Na Mwanajuma Abdi

HAJI Mussa Kitole ambaye alichukua fomu Tume ya Uchaguzi Zanzibar kuwania Urais wa Zanzibar kupitia chama cha Sauti ya Umma (SAU) ameshindwa kurejesha fomu hadi ulipofika muda wa mwisho wa kurejesha fomu hizo saa 10 jioni jana.

Akizungumza na Zanzibar Leo, Kitole alisema hakuweza kurejesha fomu hizo kwasababu chama chake cha Sauti ya Umma hakijampatia fedha za kulipa dhamana ya fomu hiyo shilingi 2,000,000.

Hata hivyo, alisema kutokana na kushindwa kuingia katika kinyang'anyiro cha Urais ameamua kujaza fomu ya kuwania nafasi ya ujumbe wa Baraza la Wawakilishi kupitia chama hicho katika jimbo la Mkwajuni, Wilaya ya Kaskazini 'A' Unguja.

Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Salum Kassim Ali alilithibitishia gazeti la Zanzibar Leo jana jioni, kwamba mgombea huyo hakurejesha fomu yake.

Hata hivyo, alieleza kuwa Kitole hajaitaarifu Tume ya Uchaguzi Zanzibar kitu chochote juu ya kushindwa kwake kurejesha fomu hiyo.

Chama cha Sauti ya Umma (SAU), kilianza mtafaruki mapema wakati wa uchukuaji fomu hiyo, baada ya wagombea wake wawili kujitokeza kwa wakati mmoja Tume ya Uchaguzi kutaka kuchukua fomu kuwania urais, jambo ambalo lilisababisha Tume ya Uchaguzi Zanzibar kuwanyima fomu hizo.

Wanachama hao Kitole na mwenzake Haji Ramadhan walishindwa kukabidhiwa foimu hizo na kushauiriwa na tume hiyo wakakae ili waweze kutoa mgombea mmoja, na baadaye Kitole kwenda kukabidhiwa fomu hiyo.

Wakati huo huo, mgombea wa Urais wa Zanzibar kupitia kwa Chama cha Jahazi Asilia, Kassim Ali Bakari jana alirejesha fomu hiyo majira ya saa 7:30 mchana, ambapo Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Khatib Mwinyichande alizipokea fomu hizo, baada ya kukamilisha taratibu za ujazaji wa fomu.

Mgombea huyo alisema pindi akipewa ridhaa ya kuongoza ataweka mbele kukuza uchumi wa nchi katika kukabiliana na soko la Afrika Mashariki pamoja na kuimarisha kilimo.

Mgombea mengine aliyerejesha fomu ya Urais wa Zanzibar kutoka Chama cha Mwamko wa Umma (NRA), Haji Khamis Haji ambae alifika majira ya saa 8:00 mchana katika Makao Makuu ya Tume hiyo kwa ajili ya kurejesha fomu hizo.

Mwenyekiti wa ZEC, Khatib Mwinyichande alipokea fomu hizo, ambapo alimpongeza kwa kuweza kurejesha fomu hizo kabla ya muda wa mwisho kumalizika.

Nae, Mgombea Haji Khamis aliipongeza ZEC kwa kufanya kazi vizuri na kuwahimiza viongozi wa tume hiyo kuendelea kusimamia sdemokrasia vizuri.

Kutokana na kung'oka kwa mgombea wa SAU, sasa wagombea Urais wa Zanzibar wamebakia saba ambao ni Dk. Ali Mohammed Shein (CCM), Maalim Seif Sharif Hamad (CUF), Haji Ambar Khamis ( NCCR Mageuzi), Juma Ali Khatib (TADEA), Said Soud (AFP), Haji Khamis Haji (NRA) na Kassim Ali Bakari wa Jahazi Asilia.

No comments:

Post a Comment