Tuesday 17 August 2010

SEIF SHARIF ACHUKUWA FOMU KUWANIA URAIS ZANZIBAR.

Seif Sharif achukua fomu kuwania urais Z'bar


Mwanajuma Abdi na Kassim Kassim, TUDARCO

KATIBU Mkuu wa CUF ambae pia ni mgombea Urais wa Zanzibar kupitia chama hicho, Seif Sharif Hamad, amesema siasa za kupakana matope na matusi hazina nafasi katika kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka huu katika kujenga Zanzibar mpya na badala yake zitafanyika za kiungwana za kupingana kwa hoja.

Hayo aliyasema jana, baada ya kuchukua fomu ya uteuzi wa mgombea Urais wa Zanzibar katika Afisi za Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Maisara, ambapo alikutana na waandishi wa habari katika ukumbi wa Baytul - Yamin, huko Bwawani mjini hapa.

Alisema kampeni za kupakana matope na kuchafuana au kubezana na kukashifiana hazitopewa nafasi katika chama hicho, ambapo pia anaimani na vyama vyengine vitaendesha kampeni za kistaarabu katika kuiendeleza Zanzibar mpya yenye matumaini ya kukuza umoja na mshikamano wa Wazanzibari wote.

Alieleza kampeni za uchaguzi wa mwaka huu zitakuwa zinalenga zaidi kushindana kwa hoja, sambamba na kuwa na imani ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) itaendesha uchaguzi mkuu kwa uhuru, uwazi na uadilifu mkubwa kama walivyofanya katika uchaguzi wa kura ya maoni, ambao umewapatia sifa kubwa ndani na nje ya nchi.

Maalim Seif alisema Agosti tisa ya mwaka huu, wananchi wa Zanzibar wameshuhudia mageuzi makubwa ya nchi yaliyofanywa na Baraza la Wawakilishi kwa kubadilisha baadhi ya vifungu vya katiba kwa kauli moja juu ya uundwaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa baada ya uchaguzi Mkuu utaofanyika Oktoba 31 mwaka huu.

Aliongeza kwamba chimbuko la mageuzi Zanzibar limetokana na mazungumzo yake aliyoyafanya na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Amani Abeid Karume Novemba 5, 2009, ambapo kwa sasa wananchi wamedumisha umoja, mshikamano na kuweka nchi katika utulivu na amani.

Alifahamisha kuwa, kwa kipindi kirefu utulivu huo ulikuwa unakosekana katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu na kwamba kuna watu wangekuwa wameshapigwa na wengine wamewekwa ndani, lakini kwa sasa hilo halipo baada ya maridhiano hayo,atayaendeleza katika kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa kitaifa.

Alisema pindi akiteuliwa na tume na kuchaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar mambo atayoyapa kipaombele katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa ni pamoja na kuimarisha Muungano kwa kuendeleza mazungumzo ya kero za muungano chini ya misingi ya haki, usawa na kuheshimiana.

Mambo mengine ni kuendeleza maridhiano ya kisiasa yaliyofikiwa Zanzibar, kujenga uchumi imara katika mfumo wa soko huria katika kunyanyua sekta za kilimo, uvuvi, utalii, biashara na viwanda pamoja na kuimarisha nidhamu ya utendaji kazi Serikalini, kuimarisha huduma za afya, maji safi na salama na kuinua viwango vya elimu katika skuli za msingi hadi vyuo vikuu ili Zanzibar iwe ndiyo kituo kikuu cha elimu na mafunzo stadi katika Afrika Mashariki.

Mapema Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Khatib Mwinyichande, akimkabidhi fomu hiyo Maalim Seif, alimpongeza kwa ujasiri wake wa kwenda kuchukua fomu hiyo.

Hata hivyo, alimsomea muongozo wa fomu hizo ikiwemo ya fomu ya uteuzi, maelezo binafsi, tamko la kisheria na kuwa na wadhamini wasiopungua 200 kutoka katika mikoa yote mitano ya Zanzibar, ambao waliojiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 31 mwaka huu na fomu hiyo siku ya mwisho kurejeshwa ni 10:00 jioni ya Agosti 30.

Nae Maalim Seif aliwapongeza ZEC kwa kuendesha kura ya maoni kwa uadilifu mkubwa na utulivu na amani, ambapo aliomba uchaguzi mkuu nao wausimamie vizuri ili uwe wazi na huru kama uchaguzi huo uliomalizika wa kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

No comments:

Post a Comment