NEC Yapokea fomu za ubunge Zanzibar
Na Mwajuma Juma
WAGOMBEA tisa wa nafasi za ubunge wamekamilisha taratibu za kurejesha fomu hizo katika Tume ya Uchaguzi ya Taifa, Wilaya ya Kati Unguja.
Wagombea hao ambao gazeti hili lilishuhudia wakirejesha fomu hizo katika wilaya hizo wakiwa kutoka vyama tofauti walirejesha fomu hizo kuanzia majira ya saa 4:00 za asubuhi katika ofisi hiyo Dunga .
Wagombea ambao walirejesha fomu hizo na majimbo wanayoyawania katika mabano walikuwa ni Mohammed Seif Khatib (Uzini), Yahya Kassim Issa (Chwaka) na Amina Andrea Clement (Koani) wote wanawania nafasi hiyo kupitia chama cha Mapinduzi (CCM).
Kwa upande wa Chama Cha Wananchi CUF ni Shaaban Iddi Ame (Koani), Ali Khamis Ame (Chwaka) na Abdi Mohammed Adeyum (Uzini), ambapo kwa upande wa TLP ni Ramadhan Soud Mlenge (Chwaka) na Issa Ame Issa (Koani), kupitia chama cha TADEA.
Kwa mujibu wa Wasimamizi wa Uchaguzi katika majimbo hayo walisema kwamba idadi hiyo ya wagombea waliorejesha fomu hizo ilikuwa ni hadi saa 7:00 mchana ambapo ilikuwa bado kuna wagombea wengine hawajarejesha fomu hizo.
Walisema kwamba zoezi la urejeshaji wa fomu hizo ilikwua ni hadi saa 10:00 za jioni ambapo baadae watabandika majina ya wagombea hao kwa ajili ya pingamizi.
"Bado tunaendelea kupokea majina ya wagombea na mwisho ni saa 10:00 za jioni ambapo baadae tutayabandika majina ya wagombea wote kwa ajili ya pingamizi", alisema Msimamizi Msaidizi wa Jimbo la Uzini Issa Suleiman Saleh.
Zoezi la uchukuaji wa fomu kwa upande wa Wabunge lilianza Agosti 15 mwaka huu na kukamilika juzi Agosti 19 mwaka huu, katika Wilaya zote za Unguja na Pemba.
Friday, 20 August 2010
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment