Pemba kichagueni CCM - Mama Shein
Zuhra Msabah, Pemba
MKE wa Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwanamwema Shein amewataka wananchi wa mkoa wa Kaskazini Pemba kukichagua chama cha Mapinduzi wakati wa uchaguzi mkuu ujao utakapowadia.
Mama Shein alisema hayo katika ukumbi wa Benjamini Mkapa Wete Pemba alipokuwa akizungumza na wajumbe UWT na akina mama wa mkoa wa Kaskazini Pemba.
Alisema chama hicho kina kila sababu ya kuchaguliwa na kushinda kwenye uchaguzi mkuu ujao, kwani kina ilani ambayo ndiyo dira ya maendeeleo kwa wananchi.
Sambamba na hilo mama Shein, alisema ilani ya chama hicho imekuwa ikitekelezwa kivitendo ambapo kila mwananchi amekuwa akishuhudia maendeleo yaliyofikiwa hapa nchini.
Mama Shein alisema wanawake wakishikana kwa umoja wao wanaweza kukiwezesha chama hicho kushinda kwa ushindi wa kishindo.
"Akina mama tunaweza lakini muhimu tushikamane na tuwe wamoja ili tuweze kupata ushindi wa kishindo",alisema mama Shein.
Alisema chama cha Mapinduzi kimekuwa kikisitiza umuhimu wa kuwapatia maendeleo wananchi wake sambamba na kuendeleza amani na utulivu ambao unawezesha wananchi hao kufanya shughuli zao bila ya bughdha.
Naye Katibu wa UWT mkoa wa Kaskazini, Mafunda Khamis Ali alisema akinamama wapatao 70 katika mkoa huo walitokeza kwa wingi kuwania nafasi mbali mbali.
Alisema kati ya hao 26 wamefanikiwa kupitishwa kuwania nafasi hizo huku wakisubiri kuingia kwenye uchaguzi mkuu.
Mafunda alisema katika mkoa huo, hali ya kisiasa imekuwa tulivu tofauti na miaka iliyopita.
Katika ziara hiyo Mama Shein alifuatana na Mke wa Waziri Kiongozi Asha Shamsi, Waziri wa Kazi, Vijana na Maendeleo ya Wanawake na Watoto, Asha Abdulla Juma na Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii ya Jamhuri ya Muungano Dk. Aisha Kigoda.
Tuesday, 24 August 2010
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment