Wahimizwa kutumia vyema fedha za miradi
Raya Hamad, Maelezo
WANANCHI na wavuvi wanaoishi katika maeneo ya ukanda wa pwani wameshauriwa kuzitumia fedha za mradi wa usimamizi wa mazingira ya bahari na ukanda wa pwani MACEMP kwa kuziwekeza katika ufugaji wa samaki katika maeneo ya Bahari.
Mkurugenzi wa Idara ya uvuvi na mazao ya baharini, Mussa Aboud Jumbe, ameyasema hayo kwenye mkutano wa mwaka uliowakutanisha wenyeviti na makatibu wa kamati tendaji za wavuvi na wakulima wa mwani wenye lengo la kutathmini mafanikio na matatizo mbali mbali.
Mussa amewataka wavuvi kuukubali mpango huo endelevu wenye tija ya uhakika wenye gharama nafuu za uwekezaji na wenye mavuno makubwa yenye faida ambao hutumia utaalamu wa kisasa kwa kupata ushauri wa wataalamu kutoka Idara ya uvuvi ili kuepuka uharibifu na uchafuzi wa mazingira .
Aidha, Mussa amesisitiza kuwa ufugaji wa viumbe wa baharini utawawezesha wavuvi kuwa na tija ya uhakika kwa vile ufugaji wake ni wa kawaida wenye gharama ndogo za uwekezaji na faida ya mavuno ni kubwa “Sisi tuna eneo kubwa la bahari na maeneo mengi ya bahari yameingia ndani hii ni faraja kubwa kwani ufugaji wa mazao ya baharini unakuwa rahisi zaidi hasa kisiwa cha Pemba”, alisema Mussa
Mussa amesema uchumi wa nchi unakua kutokana na rasilimali zilizomo nchini na ndio maana Serikali kupitia mradi wa MACEMP umekuwa ukiwawezesha wavuvi na wakulima wa mwani kwa kuwapa taaluma,kuwaweka pamoja ,na kuwapatia vifaa vya kisasa, pamoja na kuwa na uwezo wa kubuni miradi mbadala ili wakuze kipato chao na kusaidia kukuwa kwa uchumi wanchi .
Mkurugenzi huyo amesisitiza miradi ya ufugaji wa samaki itakapo imarika zaidi itatowa fursa ya pekee kwa wawekezaji wa ndani na wanje kuweza kuja kuwekeza hapa nchini na hivyo kuwa na ongezeko la ajira .
Akitowa mada kuhusu ufugaji wa viumbe vya baharini, Hashim Moumin amesema wakati umefika kwa wavuvi kubadilisha mfumo uliopo wa wavuvi wote kutegemea bahari pekee bali wajikite zaidi na ufugaji wa viumbe wa baharini kwa lengo la kuinuwa kipato cha mvuvi na kuondokana na umasilikni
Hashim amesema ufugaji wa viumbe wa baharini sio jambo geni hapa visiwani lakini bado mwamko ni mdogo hivyo amewataka wavuvi kujitahidi kujikita katika ufugaji wa viumbe wa baharini zaidi ili kuepusha msongamano wa wavuvi na wakulima wa mwani wanaokwenda baharini.
Miongoni mwa nchi zinazojishughulisha na ufugaji wa samaki ni pamoja na China, Norway, Japan, Indonesia Philipine, Korea ambazo zimepata mafanikio makubwa kwa kukuza kipato cha wavuvi ,na kukuza uchumi nchi zao.
Mkutano huo ulifunguliwa na Afisa Mdhamini wa Wizara ya Kilimo Mifugo na Mazingira na kuhudhuriwa na Wakuu wote wa Wilaya za Pemba,Maafisa Tawala, Wataalamu kutoka Idara ya Uvuvi, Meneja wa Mradi wa Mradi wa MACEMP na watendaji wake .
Monday, 30 August 2010
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment