ZATI kujadili changamoto za utalii
Na Salum Vuai, Maelezo
JUMUIA ya Wawekezaji wa Sekta ya Utalii Zanzibar (ZATI), asubuhi hii inatarajia kufanya mkutano maalumu utakaojadili changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo.
Mkutano huo umepangwa kufanyika katika hoteli ya Serena Inn kuanzia saa 3 za asubuhi ambapo wajumbe wa bodi ya jumuia hiyo watakutana na watendaji wakuu wa taasisi nyengine za serikali kutafuta njia za kutatua matatizo yanayojitokeza katika biashara ya utalii hapa nchini.
Mwenyekiti wa jumuia hiyo Simai Mohammed Said alilieleza gazeti hili kuwa, kumekuwa na changamoto nyingi zinazohitaji kufanyiwa kazi katika mikakati ya kuimarisha utalii wa Zanzibar, ambazo nyengine zimekuwa zikielezwa na wadau wa sekta hiyo kupitia vyanzo tafauti zikiwemo warsha zinazohusu biashara ya utalii.
Alizitaja kuwa ni pamoja na suala zima la usalama wa wageni katika maeneo mbalimbali zikiwemo fukwe sambamba na kero ya mapapasi ambao kwa njia moja au nyengine wanachangia kuleta taswira mbaya kwa watalii wanaotembelea nchini.
Aidha alisema jambo jengine ni kufanya upembuzi wa malalamiko ya kuwepo utaratibu usioridhisha wa mikataba kati ya waajiri na wafanyakazi wa mahoteli, mikahawa ya kitalii na mengineyo yanayohusiana na sekta hiyo.
Said alisema mkutano huo utahudhuriwa na watendaji wa sekta mbalimbali ikiwa pamoja na Mkurugenzi wa Masoko katika Kamisheni ya Utalii, Mkuu wa Idara ya Uhamiaji, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Rais wa Jumuia ya Wafanyabiashara, wenye viwanda na wakulima Zanzibar na wengineo.
Alisema mwisho wa kikao hicho kinachokadiriwa kuchukua muda wa saa nne, kutatolewa mapendekezo ya njia za kuimarisha utalii kwa kuzifanyia kazi kero mbalimbali zitakazoibuliwa.
ZATI imekuwa na utaratibu huo kila mwaka, ambapo imekuwa ikikutana na wadau wa taasisi za umma zinazohusika kwa njia moja au nyengine katika kuimarisha sekta ya utalii nchini.
Tuesday, 24 August 2010
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment