Tuesday, 17 August 2010

WAISLAMU WAKRISTO WAGOMBEA MAITI HOSPITALI YA MNAZI MMOJA.

Waislamu, Wakristo wagombea maiti Mnazimmoja


Saada Mamboleo na Hasina Rashid, MCC

MVUTANO mkubwa umejitokeza katika hospitali kuu ya Mnazimmoja mjini hapa jana katika kugombea maiti kati ya waislam na wakristo.

Akizungumza na mwandishi wa gazeti hili, rafiki wa karibu wa marehemu Fadhil Abdalla Kisongwe, alisema marehemu Daud Jon Luta (39) aliekuwa akiishi Michenzani nyumba nambari 3 alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya kifua kikuu na alifarki dunia Agosti 16 saa 8 kasorobo mchana katika hospitali ya Mnazimmoja.

Alisema marehemu Daud alikuwa muislamu kwa mujibu wa maneno yake alipokuwa hai na inasemekana alisilimishwa na sheikh Jamhuri ambae yupo nje ya kisiwa cha Zanzibar kwa hivi sasa.

Hata hivyo, Sheikh huyo hakuweza kupatikana mara moja kuzungumzia madai hayo

Rafiki huyo, alifahamisha kwamba kabla ya Daud kupatwa na kifo alimuuliza "wewe ni muislamu, akakiri ndio lakini akamuuliza tena na kumshauri kama muislamu kweli atoe shahada.

Alisema baada ya kumwambia hivyo, marehemu akashahadia lakini kwa matamshi yake hayakutoka uzuri kutokana na kutofahamu sana lugha ya kiswahili.

"Ilipofika Augosti 16 asubuhi nilimuuliza una dini gani?

akasema mimi ni muislam..halafu nikamwambia ashahadie nae marehem akashahadia, "Alisisitiza rafiki huyo, Fadhil Abdallah Kisongwe.

Rafiki huyo ambae ni muislamu akiongoza kundi la waislamu na majirani wa marehemu, walilenga kumchukua maiti huyo kwa kumkosha na kufanyia ada zote za maiti na halafu wamzike kiislamu kutokana na kuamini kwao kwamba alikwa muislamu

kutokana na kauli zake wakati wa uhai wake.

Habari za uchunguzi ambazo waandishi wa habari walizipata zinasema kwamba wakati marehemu akigua, majirani pamoja na rafiki yake waliwaarifu jamaa wa marehemu kuhusu hali yake lakini hawakujtokeza.

Aidha, majirani hao waliwaarifu tena ndugu wa marehemu juu ya kifo chake na walipofika walitaka kumchukua na kumzika kwa dini ya kikristo, jambo ambalo majirani na marafiki walikataa, asizikwe kwa dini nyengine zadi ya kiislamu kutokana na maelezo mbali mbali aliyokua akiyatoa kwa marafiki wakati wa uhai wake.

Kikundi hicho cha waislamu kilisema lengo halikuwa kugombea maiti lakini walitaka kumsitiri kwa vile ni muislamu mwenzao.

Nae kaka wa marehemu, Joseph Jon Luta alisema marehemu huyo alikuwa ni mkristo tokea mdogo na cheti chake cha ubatizo anacho.

Alisema alijaribu kuomba uthibitisho kwa majirani hao kama marehemu alikuwa amesilimu lakini haukupatikana uthibitisho wowote.

Kaka huyo alisema yeye na wadogo zake hawataki malumbano na kutangaza kujitoa katika kushughulikia mwili wa marehemu lakini katika mazishi watashiriki.

Hata hivyo, ndugu huyo alidai kuwa waislam wametumia nguvu kuwanyang’anya maiti wa ndugu yao kutokana na wingi wa waislam na wao wakristo walikuwa wachache.

Hatimae mzozo huo, ulimalizika kwa waislamu kumchukua maiti na kufanyia ada zote na kumzika katika makaburi ya waislamu Mwanakwerekwe.

No comments:

Post a Comment