Wednesday, 25 August 2010

DK, SHEIN WANACCM PEMBA PUUZENI GHILBA ZINAZOENEZWA.

Dk.Sheni: Wana CCM Pemba puuzeni ghilba zinazoenezwa

 Ni madai ukipigia kura upinzani sawa na umempigia yeye


 Nahodha ataka kambi zivunjwe auungwe mkono Dk. sheni


Abdulla A. Abdulla, Pemba

MGOMBEA urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk. Ali Mohammed Shein amewasihi wanachama, wapenzi na wananchi kisiwani Pemba kutoghilibika na kauli za wapinzani zinazodai kuwa kuwapigia kura wapinzani ni sawa na kumpigia kura Dk. Sheni.

Dk. Shein alisema hayo huko Mkoani, Kusini pemba katika siku ya mwisho ya ziara yake ya siku tatu Kisiwani Pemba ya kuzungumza na viongozi wa CCM wa ngazi mbali mbali katika chama hicho.

Alisema tayari wapinzani wake wameshaanza kupiga kampeni za nyumba kwa nyumba na kuwaeleza wananchi kuwa kutokana na maridhiano yaliyopo hivi sasa wakimpa kura mpinzani ni sawa na kumpa Dk. Sheni, jambo ambalo halina ukweli.

Aidha, mgombea huyo alisema chama CCM mwaka huu kinakusudia kufanya kampeni za kiistaarabu zenye lengo la kudumisha amani na kuepusha bughudha mitaani.

Wakati huo huo, Waziri Kiongozi wa Zanzibar na Mlezi wa Chama cha CCM katika Mkoa wa Kaskazini Pemba, Shamsi Vuai Nahodha alitaka kundi lililokuwa likimuunga mkono alipokuwa akiwania urais livunjike na limuunge mkono Dk. Sheni.

Nahodha aliyasema hayo alipokuwa akitoa salamu za shukrani kwa niaba ya viongozi wa Mkoa huo katika mkutano wa Mgombea Urais huyo na viongozi wa Chama wa ngazi mbali mbali uliofanyika Micheweni.

Nahodha alisema, Dk. Ali Mohammed Shein ni kiongozi makini, mwenye uwezo mkubwa na uzoefu wa muda mrefu wa kuongoza, hivyo chama hakikufanya makosa kumteuwa kupeperusha bendera ya Zanzibar.

“Ushindi wa CCM ni ushindi wetu sote wala hatutopoteza, iwapo Dk. Shein atashinda na kuwa Rais wa Zanzibar kwani yeye ni Mwana CCM”, alisema Nahodha.

Waziri Kiongozi alisisitiza kuwa CCM ina viongozi wazuri wengi wanaofaa kwa sasa na baadaye, hivyo kumuunga mkono Dk. Shein ni kuendelea kuwekeza ili kurahisisha urithi wa madaraka baada ya kumaliza muda wake wa uongozi.

No comments:

Post a Comment