Thursday 19 August 2010

MANISPAA YAKIRI ASKARI WAKE KUCHUKUA RUSHWA.

      Manispaa yakiri askari wake kuchukua rushwa


Na Khamisuu Abdalla (MCC)

BARAZA la Manispaa limesema kuwa baadhi ya askari wake wamejenga tabia mbaya ya kuomba na kuchukua rushwa kutoka kwa wafanyabiashara mbali mbali.

Mkuu wa soko kuu la Darajani, Fadhil Khatib Shaban amethibitisha kuwepo kwa tabia hiyo kwa baadhi ya askari wa Baraza hilo.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, afisini kwake Darajani, Shaaban alisema, askari hao hawawajibiki ipasavyo katika kazi badala yake wanachukua rushwa ya pesa au bidhaa kutoka kwa wafanya biashara hao.

Fadhil alisema uchunguzi uliofanywa na Baraza lake umethibitika na kuhakikisha kwamba baadhi ya askari wanachukua rushwa hizo.

Aidha, alifahamisha kwamba katika kukabiliana na tatizo hilo baraza lake linakusudia kuchukua hatua ya kuwabadilishia maeneo ya kazi ili kujaribu kupunguza malalamiko hayo ya wananchi.

Hata hivyo, Mkuu huyo wa soko la Darajani, hakutaka kutaja majina ya askari hao waliobainika kuwa na tabia hiyo au hatua za kisheria walizochukuliwa kutokana na vitendo hivyo vya rushwa.

Kuhusu wafanyabiashara wanaoendesha biashara zao katika maeneo yasiyoruhusiwa, Fadhil alisema baraza lake litaendelea kuwachukulia hatua kali za kisheria pamoja na kuwafikisha katika mahakama ya baraza hilo lilioko Malindi.

Alisema wafanyabiashara hao wanaharibu mazingira katika mji wa Zanzibar kwani jukumu la kudumisha usafi sio la baraza la Manispaa peke yake na kwamba kila mtu wakiwemo wafanyabiashara wanapaswa kuweka mazingira safi hasa kwa maeneo wanayofanyiabiashara zao na kwamba Baraza halitaridhia mtu yeyote kuchafua mji wa Zanzibar.

No comments:

Post a Comment