Friday 27 August 2010

Huzuni Zatawala Kifo Cha Mufti Mkuu wa Zanzibar.

Huzuni zatawala kifo cha Mufti Mkuu Zanzibar


Alikuwa matibabuni India
Anatarajia kuzikwa kesho

Na Mwanajuma Abdi

MUFTI Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Harith bin Khelef Khamis amefariki dunia alfajiri ya kuamkia jana katika hospitali ya Meyot, Mjini Chenay, India.

Katika mahojiano na gazeti hili jana, mmoja wa watu wa familia yake, Abdallah Seif Khelef Khamis, akizungumza kutoka nyumbani kwa marehemu Migombani mjini hapa, alisema Marehemu alifariki dunia kati ya saa 10:00 na 10:24 alfajiri katika hospitali Meyot Chenay nchini India alikokuwa amelazwa.

Alisema Marehemu Sheikh Khelef alipelekwa matibabuni India wiki tatu zilizopita na kufikwa na mauti alfajiri ya jana.

Aidha, aliongeza kwa kusema kabla ya mauti yake, alifanyiwa upasuaji mdogo wa kibofu cha mkojo ambapo baadae alfajiri wanafamilia hao walijulishwa juu ya habari za msiba huo kwa njia ya simu.

Nae Katibu wa Mufti Mkuu Zanzibar, Sheikh Fadhil Soraga akitoa taarifa ya kifo hicho kwa vyombo vya habari, alifahamisha kuwa, nchi imepatwa na msiba mkubwa kwa kuondokewa na kiongozi wa dini visiwani, ambae alikuwa matibabuni India.

"Taarifa juu ya kifo cha Mheshimiwa Mufti Mkuu wa Zanzibar zimepokelewa alfajiri ya jana na mipango ya kusafirisha mwili wa marehemu inaendelea kwa mashirikiano makubwa na ubalozi wetu nchini India," Alisema Sheikh Soraga.

Aidha, Soraga alisema maandalizi ya kuupokea mwili wa marehemu kwa heshima zote za kitaifa unaendelea na wananchi watajuulishwa kuwasili kwa maiti na siku ya maziko muda utakapofika", alifafanua Sheikh Soraga.

Hata hivyo, taarifa zilizotolewa na kiongozi mmoja

wa msikiti wa Mushawar, Mwembeshauri zilieleza kuwa mwili wa marehemu ulitarajiwa kuondoka India jana kupitia Qatar na baadae kuwasili Dar -es salaam.

Alisema maziko ya marehemu yanatarajiwa kufanyika kesho Jumapili.

Sheikh Soraga aliwataka waumini na wananchi wote kwa ujumla kuwa watulivu na kuungana pamoja katika kuukabili msiba huo mkubwa wa kitaifa, ambapo alisisitiza kubwa zaidi ni kumuombea Marehemu maghfira kwa Mwenyezi Mungu ili amlaze mahali pema peponi aamin.

Alisema Serikali iko pamoja na wafiwa wote katika msiba huo mkubwa na anawaomba wawe na subira katika kupokea qadar ya Mwenyezi Mungu.

Mufti Mkuu wa Zanzibar ameacha kizuka mmoja.

No comments:

Post a Comment