Tuesday, 17 August 2010

WAWILI WA CHAMA KIMOJA YAJITOKEZA KUCHUKUWA FOMU YA URAIS TUME YA UCHAGUZI ZANZIBAR.

Wawili Sauti ya Umma wakumbana ZEC kugombania fomu ya Urais

ZEC yawakatalia, yataka warudi Chamani kujipanga

Said Soud kugombea Urais kupitia Chama cha Wakulima

Kassim Kassim TUDARCO na Mwanajuma Abdi

TUME ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), imewanyima fomu wagombea wawili wa chama cha Sauti ya Umma, Haji Ramadhan Haji na Haji Mussa Kitole, baada ya kujitokeza kwa pamoja kuchukua fomu ya uteuzi wa kuwania urais wa Zanzibar katika uchaguzi mkuu ujao na badala yake kuwaelekeza warudi katika chama na kuleta jina moja.

Kunyimwa huko kumefuatia chama hicho kukiuka utaratibu wa Tume hiyo ya kumpatia fomu ya Urais mgombea mmoja kutoka kila chama kitachosimamisha mgombea urais wa Zanzibar, lakini badala yake chama hicho kimepeleka barua mbili za majina ya wagombea wawili kwa siku tofauti ya Agosti 12 na Agosti 13 mwaka huu katika Afisi za ZEC.

Akizungumza wagombea na waandishi wa habari waliofika katika Afisi za ZEC, Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Salum Kassim Ali, alisema haiwezekani kukabidhiwa fomu wagombea wawili ndani ya chama kimoja ya Urais wa Zanzibar.

"Chama cha Sauti ya Umma kilileta barua ya kwanza Agosti 12 mwaka huu iliyomuonesha jina la Haji Mussa Kitole kuwa ni mgombea wa urais kwa tiketi ya chama, lakini cha ajabu siku ya pili ya Agosti 13, ZEC imepokea barua nyengine iliyomtaja mgombea Haji Ramadhan Haji bila ya kufuta barua ya kwanza, wala hakuna sababu yoyote iliyoainishwa kutokana na hali hiyo hatuwezi kutoa fomu kwa wagombea wawili kwa chama kimoja ni bora murudi katika chama chenu wa kuendelea na mchakato wa kutafuta mgombea mmoja na barua isainiwe na Katibu Mkuu au Naibu Katibu Mkuu", alifafanua Salum.

Wagombea hao wakizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Haji Ramadhan Haji, ambae ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Taifa, alisema jina la kugombea nafasi hiyo limepitishwa katika kikao halali kilichofanyika Zanzibar baada ya kumaliza kwa mkutano mkuu uliofanyika Juni 25, Jijini Dar es Salaam.

Alieleza anashangazwa na kuona barua ya Haji Mussa Kitole kuwa anagombea nafasi hiyo jana mbele ya Mkurugenzi wa Tume wakati chama hakijampitisha kuwa mgombea wa nafasi hiyo, ambapo katika mkutano mkuu alitangaza nia tu.

Nae Haji Mussa Kitole, alisema amepitishwa na mkutano mkuu wa Chama hicho uliofanyika Jijini Dar es Salaam alichoteuliwa kuwania nafasi ya urais Zanzibar pamoja na kutangazwa kuwa Makamo Mwenyekiti wa Sauti ya Umma Zanzibar, lakini anashangazwa kuona Haji Ramadhan Haji amejitokeza kuwania nafasi hiyo.

Nae Mwantanga Ame anaripoti kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wakulima na Wafanyakazi na wenye Viwanda Zanzibar (AFP), Said Soud, amejitokeza kuchukua fomu kwa ajili ya kuwania urais wa Zanzibar katika uchaguzi ujao.

Soud, alichuku fomu hiyo jana Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), baada ya kukabidhiwa rasmi na Mwenyekiti wa Tume hiyo Khatib Mwinchande huko Afisini kwake Maisara Mjini Zanzibar.

Akitoa maelezo yake baada ya kukabidhi fomu hiyo Mwenyekiti huyo alimpongeza kwa hatua ya kuamua kuchukua fomu hiyo na kumtaka Makamu huyo kuhakikisha kuwa anazijaza kwa usahihi huku akizirejesha kwa wakati.



Mwenyekiti huyo alisema kuwa hatua ya chama hicho kutimiza azma ya kuchukua fomu hiyo baada ya hapo awali kuahidi kufanya hivyo ilikuwa ni ya kupongezwa kutokana na baadhi ya vyama kuwasilisha maombi ya kuchukua fomu hizo, lakini zimeshindwa kufanya hivyo jambo ambalo Chama hicho alikieleza kimekuwa kiungwana kutimiza ahadi zake.

Naye Makamu Mwenyekiti huyo akitoa shukrani zake kwa Tume hiyo, aliipongeza kutokana na kuweza kujipanga vyema katika uchaguzi Mkuu ujao na kuitaka kuhakikisha wanatenda haki katika uchaguzi ujao.

Alisema haitakuwa busara kuona Tume hiyo ikiwa imo katika uendeshaji wa uchaguzi ujao ukawunaegemea katika kukipa haki chama kimoja ama viwili pekee.

Aidha Mgombea huyo akizungumza na waandishi wa habari katika Afisi za ZEC, alisema madhumuni ya kuwania nafasi hiyo ni kuona chama chao kinashiriki kuwajali a Zanzibari katika kuwapatia mambo mbali mbali ya msingi ili maisha yao yaweze kuwa yenye maendeleo.

Alisema Chama hicho katika mambo ambayo imeyaandaa katika ilani yake ni pamoja na kukuza ajira kwa vijana hasa sekta ya viwanda, pamoja na kukuza kilimo kwa kukifanya kuwa cha kisasa kwa vile nguvu kazi ya kutimiza hilo bado ipo nchini.

Alisema inasikitisha kuona Zanzibar ikiwa bado ina eneo kubwa kwa ajili ya kutumika kwa shughuli za kilimo lakini sehemu kubwa ya chakula cha wazanzibari kimekuwa kikiagizwa kutoka nje jambo ambalo limekuwa likisababisha kupotea kwa fedha nyingi zinazokusanywa katika mapato ya ndani.

Akiendelea alisema katika muundo wa serikali yake anakusudia kuwapa kipaumbele wanawake kwa kuwapatia nafasi za juu za uongozi kwa vile ni moja ya sera ya Chama chao huku akikitahadharisha Chama cha CUF kuwa mwaka huu hawatakuwa na mchezo wa kujenga muungano kwa ajili ya kukisaidia kama kilivyokuwakikifanyakatika chaguzi zilizopita.

Makamu huyo alisema muundo wa serikali yake utakuwa ni serikali tatu, lakini atahkikisha Muungano unabakia bali atajitahidi kuondoa baadhi ya kero za Muungano ambazo zimekuwa zikijitokeza mara kwa mara.

Soud alifahamisha kuwa chama chake katika uchaguzi Mkuu ujao kinakusudia kusimamisha wagombea 50 ambapo kwa upande wa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi ni wagombea 25 na Ubunge ni 25 ambao watakuwa ni kwa Unguja na Pemba.

Wakati Mgombea huyo akiwasili katika viunga vya tume ya Uchaguzi ya Zanzibar alisindikizwa akiwa na ulinzi wa hali ya juu wa vijana wa Chama chake waliokuwa wamevalia fulana zenye ujumbe ulikokuwa ukisomeka kuwa 'siasa safi ni uwajibikaji, mabadiliko ni lazima 'full' kujiachia'.

No comments:

Post a Comment