Tuvunje makundi na kubakia na kundi moja tu la CCM - Dk. Shein
Mwandishi Maalum
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Ali Mohammed Shein, amewataka wanaCCM kutambua kuwa kazi kubwa iliyo mbele yao hivi sasa ni kuhakikisha kuwa chama hicho kinapata ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu ujao.
Dk. Shein ambaye ni mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM ameyasema hayo kwa nyakati tofauti wakati alipokuwa akizungumza na viongozi wa mbalimbali wa CCM katika wilaya za Kusini na Kati katika mkoa wa Kusini Unguja.
Alisema sababu za kushinda zinatokana na uamuzi wa chama kwa mujibu wa Katiba yake na jinsi CCM ilivyojipanga.
Dk. Shein alisema kauli ya chama hicho ya ushindi ni lazima inayotokana na agizo la chama katika Ibara ya 5 kifungu kidogo cha kwanza cha Katiba ya chama, ambacho kinasema inapofika wakati wa uchaguzi jukumu lake la kwanza ni kuhakikisha kinashinda uchaguzi na kushika dola ni dalili nzuri za ushindi wa chama hicho.
Akifafanua zaidi alisema ushindi huo unatokana na chama hicho kujivunia mtaji mkubwa wa watu wanaokiunga mkono chama hicho, sera nzuri na utekelezaji mzuri wa Ilani yake.
Aliwapongeza wanaCCM kwa kazi nzuri waliyoifanya ya kuchagua wagombea ndani ya chama hicho ambao ni makini katika kuleta maendeleo.
Alibainisha idadi kubwa ya wanaCCM waliojitokeza mwaka huu katika kuwania kuteuliwa nafasi mbali mbali za ubunge, uwakilishi na udiwani inadhihirisha kupanuka kwa demokrasia ndani ya chama.
Aliwataka wanaCCM kwa mara nyingine kuvunja makundi na kujenga kundi moja kwa lengo la kukipatia ushindi Chama Cha Mapinduzi.
“Wakati wa kuunga mkono mtu mmoja umekwisha, tuna kundi moja la CCM…hapa lengo ni kupata ushindi na ndio jambo la msingi. Tumepewa dhamana na chama chetu, hatuwezi kwenda kinyume na taratibu za chama,” alisema Dk. Shein.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment