Tuesday 24 August 2010

CUF YAPATA PIGO

CUF yapata pigo



 Wagombea wake wawili wafariki dunia

Na Mwantanga Ame, ZJMMC

WAGOMBEA wawili wa nafasi za ujumbe wa Baraza la Wawakilishi na Udiwani kwenye uchaguzi mkuu ujao wa mwezi Oktoba mwaka huu, kupitia chama cha CUF, wamefariki dunia.

Wagombea hao ni aliyekuwa Mwakilishi wa Jimbo la Kojani, Omar Ali Jadi, aliefariki katika hospitali ya Chake Chake baada ya kusumbuliwa na ugonjwa wa ini kwa muda mrefu, na aliyekuwa mgombea Udiwani wa Wadi ya Kilimani, jimbo la Kikwajuni, Shani Ahamada Shani aliyefariki kwa ajali ya barabarani juzi.

Jadi alikuwa Mwakilishi wa Jimbo Kojani tangu mwaka 1995 na katika kipindi cha miaka 20 aliyoteuliwa kuwa Mwakilishi na miaka mitano kati ya hiyo alikuwa ni miongoni mwa Wawakilishi waliofukuzwa baada yakushindwa kuingia katika vikao vitatu mfululizo kutokana na msimamo wa chama hicho kususia matokeo ya uchaguzi huo.

Mbali ya kuwa Mwakilishi wa Jimbo la Kojani, Jadi pia alikuwa ni Mjumbe wa Mkutano mkuu Taifa wa CUF na pia alikuwa ni Mjumbe wa Mkutano mkuu wa Wilaya ya Wete Pemba.

Katika baraza la Wawakilishi lililovunjwa hivi karibuni Jadi alikuwa mjumbe wa kamati ya Baraza la Wawakilishi ya Mawasiliano na Ujenzi.

Akizungumza na Zanzibar Leo, Mkurugenzi wa Uenezi na Mawasiliano ya Umma wa CUF, Salum Bimani alisema Mwakilishi huyo alifariki juzi usiku alipokuwa akipatiwa matibabu katika hospitali hiyo ya Chake Chake.

Alisema CUF imepokea taarifa ya vifo hivyo kwa masikitiko makubwa kutokana na kutegemea mchango wa Mwakilishi pamoja na mgombea Udiwani kuendeleza Changamoto katika chama hicho katika kukipatia ushindi katika uchaguzi Mkuu ujao.

"Kifo ni mapenzi ya Mungu, lakini tumepata pigo kubwa sana kwani alikuwa Wagombea wetu walikuwa ni changamoto muhimu kwa uchaguzi Mkuu ujao" alisema Msemaji huyo.

Bimani alisema Jadi, alikuwa tayari ameshapitishwa na wananchi wa Jimbo la Kojani na Baraza Kuu la CUF, kukiwakilisha chama hicho kwenye uchaguzi mkuu ujao jambo ambalo litawatia huzuni kwa wananchi wa Jimbo hilo.

Hapo awali msemaji huyo alifahamisha kutokana na ugonjwa huo kumsumbua kwa muda Mwakilisi huyo aliweza kupatiwa matibabu na Afisi ya Baraza la Wawakilishi kaika Hospitali za Tanzania Bara katika pindi cha mienzi minne iliopita.

Alisema kutokana na kifo cha Mgombea huyo chama hicho kitamsimamisha Hamad Omar Hamad, aliyechukua nafasi ya pili kwenye kura ya maoni.

Alisema hadi anafariki Mwakilishi huyo alikuwa tayari ameshachukua fomu Afisi za Tume ya Uchaguzi Wilaya Kisiwani Pemba kwa ajili ya kuomba kuwania Jimbo hilo na alikuwa bado hajairejesha.

Mazishi ya Jadi ylifanyika jana huko Kojani ambapo Spika wa Baraza hilo aliyemaliza muda wake, Pandu Ameir Kificho, katibu wa Baraza Ibrahim Mzee na maofisa wa baraza hilo walihudhuria mazishi hayo, huku Chama cha CUF kiliwakilishwa na Makamu Mwenyekiti wake, Machano Khamis Ali.

Katika hatua nyengine Bimani alifahamisha kuwa aliyekuwa mgombea wa Udiwani Jimbo la Kikwajuni, Shani Ahmada Shani,(63), Mkaazi wa Miembeni Mjini Unguja, amefariki dunia baada ya kugongwa na gari wakati akielekea ofisi za Tume ya Uchaguzi Zanzibar kurejesha fomu yake baada ya kuijaza.

Tukio hilo limethibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharib, Aziz Juma ambapo alisema kuwa Polisi bado wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.

Wakati huo huo mtu mmoja Mkaazi wa meli nane Jecha Haji Khamis, amefariki dunia baada ya kugongwa na gari lenye namba Z 497 AL aina ya Escudo katika eneo la Bububu Wilaya ya Mjini Unguja.

Kamanda Aziz, alithibitisha kutokea kwa ajili hiyo ambapo alieleza kuwa mtu huyo aligongwa na gari hilo lililokuwa likiendeshwa na Matendo Andrew Mgeni saa 3:30 za asubuhi juzi.

Kamanda huyo alisema kuwa watuhumiwa wote wapo mikononi mwa Polisi wakiendela kufanyiwa uchunguzi ili kujua chanzo cha ajali hiyo.

No comments:

Post a Comment