Wednesday 18 August 2010

DK. KARUME AREJEA NCHINI AKITOKEA NAMIBIA.

Dk.Karume arejea nchini akitokea Namibia


Na Mwanajuma Abdi

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Amani Abeid Karume akiwa na mkewe Mama Shadya Karume wamerejea nchini jana wakitokea Namibia kuhudhuria mkutano wa 30 wa viongozi wakuu wa Nchi na Serikali za Jumuiya ya ushirikiano Kusini mwa Afrika SADC.

Rais Karume alilakiwa Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abeid Amani Karume na viongozi mbali mbali wa Serikali na chama.

Rais Karume alieshiriki mkutano huo akimuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, pia alishiriki katika sherehe za maamdhimisho ya miaka 30 tokea kuanzishwa SADC.

Nae Mama Shadya Karume, alizungumza katika mkutano huo akiwa na wake wa wakuu wa Nchi za SADC, ambapo alieleza mafanikio na changamoto zinazowakabili wanawake wa Zanzibar.

Mama Shadya aliueleza mkutano huo kuwa wanawake wa Zanzibar wamepiga hatua kubwa kimaendeleo, ambapo wamekuwa wakishiriki katika sekta zote za maendeleo, sawa na wanaume.

Aidha alisema watoto wa kike wa Zanzibar wanapata fursa sawa za kielimu na watoto wa kiume, ambapo wote waliofikia umri wa kwenda skuli wanapata fursa hiyo, huku huduma za uzazi salama wa mama na mtoto zikiendelea kuimarishwa Mijini na Vijijini.

Katika ziara hiyo, Dk. Karume, alifuatana na Waziri wa Nchi, Afisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi anayeshughulikia Fedha na Uchumi, Dk. Mwinyihaji Makame pamoja na Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mohammed Aboud.



Waziri Kiongozi wa Zanzibar, Shamsi Vuai Nahodha na Naibu waziri Kiongozi na waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Ali Juma Shamuhuna, waliongoza wananchi mbali mbali waliojitokeza kumlaki Rais Karume na mkewe, Mama Shadya Karume.

No comments:

Post a Comment